Rais Ruto alivyomeza chambo kitamu China
BAADA ya kuzima mikopo na ufadhili wa kima kikubwa kwa Afrika, China imerudi tena barani humu kwa kuirushia chambo ambacho ni vigumu kukosa kukimeza.
Tayari, Rais William Ruto aliyekuwa miongoni mwa marais wa Afrika waliohudhuria kongamano la Ushirikiano wa Afrika na China wiki hii, amepata hakikisho kuwa Kenya itapata soko la mazao ya kilimo China, nchi ambayo imefungua tena mifereji ya madeni kwa nchi za bara Afrika.
China ilipunguza mikopo kwa bara la Afrika kufuatia janga la Covid 19 lililoanzia nchini humo kabla ya kusambaa na kuathiri uchumi wa dunia na kufanya nchi nyingi za bara kukumbwa na hatari ya kushindwa kulipa madeni yake.
Katika kongamano la mwaka huu jijini Beijing, Rais wa China Xi Jinping alitangaza mpango wa utekelezaji wa ushirikiano barani Afrika wa kima cha Sh6.5 trilioni ambazo wadadisi wanasema mataifa ya Afrika yatang’ang’ania bila kujali athari zake kwa uchumi hafifu wa bara.
“China inabadilisha mwelekeo wake wa ushirikiano na Afrika wakati mataifa mengi likiwemo Kenya yanahitaji ufadhili ambao sio rahisi kupata mataifa ya magharibi kutokana na uchumi hafifu na unaoyumba. Hii ndiyo sababu inapunguza masharti ya mikopo likiwemo kutoa muda mrefu wa kuyalipa,” asema mdadisi wa masuala ya uchumi Debby Matolo.
Akifahamu mataifa mengi ya Afrika yanategemea mikopo kudumisha uthabiti wake, Rais Xi Jinping alitangaza mpango wa miaka mitatu ambao nchi yake itatumia matrilioni ya pesa barani Afrika.
Wadadisi wanasema mengi ya mataifa ya Afrika yanayolengwa na China katika mpango huu yatafanya uchaguzi ndani ya miaka mitatu ijayo ikiwemo Kenya ambayo inatarajiwa kuchagua serikali mpya mwaka wa 2027.
Katika hotuba yake kwa marais wa Afrika, kiongozi huyo wa nchi ya pili yenye uwezo mkubwa wa kiuchumi ulimwenguni alisema China inalenga kuboresha viwanda, kilimo, biashara, uwekezaji, mafunzo na miundombinu.
Mengine ni upatikanaji wa bidhaa za Afrika katika soko la China, miradi 30 ya kuunganisha miundombinu na ushirikiano wa maendeleo unaojumuisha mipango 1,000 ya kujikimu kimaisha.
‘Katika miaka mitatu ijayo, China itafanya kazi na Afrika kupitia hatua 10 ili kuimarisha ushirikiano kati ya China,” alisema.
Kati ya Sh6.5 trilioni ambazo China inapanga kuwekeza Afrika katika miaka mitatu ijayo zaidi ya asilimia nane ni mikopo huku asilimia mbili ikipitia kampuni za nchi hiyo ziwekeze barani humu.
Akionekana kushawishi marais wa Afrika kukumbatia China kwa mikopo inayolenga kubadilisha maisha ya raia, kiongozi huyo wa China alisema nchi yake na Afrika kwa pamoja zinachangia theluthi moja ya watu wote duniani, akisema bila ya pande zote mbili kuwa na maisha ya kisasa, hakuwezi kuwa na usasa kimataifa.
Alisema mpango huo wenye vipengele 10 utaafikiwa kwa ushirikiano katika utawala, kubadilishana uzoefu, mitandao ya maarifa na programu za mafunzo ya uongozi.
Rais Xi pia alisema lengo la mwelekeo huo mpya ni kukuza fursa za kiuchumi kwa nchi zinazoendelea barani Afrika, kupanua upatikanaji wa soko la bidhaa za kilimo na kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi.
Kiongozi huyo alisema hatua za ushirikiano pia zinalenga ushirikiano wa viwanda, kuimarisha teknolojia ya kidijitali na kutekeleza miradi ya uunganishaji kama vile maendeleo ya miundombinu ili kusaidia ukuaji wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika.
Zaidi ya hayo, Rais Xi alisema China inapanga kujihusisha katika uboreshaji wa sekta ya afya kwa kuanzisha ushirikiano wa matibabu, kutuma wafanyakazi wa matibabu na kusaidia sekta ya dawa barani Afrika.
‘China iko tayari kuzindua miradi 30 ya nishati safi barani Afrika, kuweka mifumo ya tahadhari ya mapema ya hali ya hewa na kufanya ushirikiano katika kuzuia maafa, kupunguza na kutoa misaada pamoja na uhifadhi wa viumbe hai,’ alisema.
Usalama
Kuhusu usalama, alisema, China itatoa msaada wa kijeshi, mafunzo na kufanya mazoezi ya pamoja ili kuimarisha juhudi za ushirikiano za usalama na Afrika.
“Tutaipa Afrika Sh18.2 bilioni za ruzuku kama usaidizi wa kijeshi, kutoa mafunzo kwa wanajeshi 6,000 na maafisa 1,000 wa polisi na watekelezaji sheria kutoka Afrika, na kuwaalika maafisa 500 wa kijeshi wa Kiafrika kuzuru Uchina,” akasema.
Hata kabla ya kongamano kuanza, Rais Ruto aliweka msingi wa ufufuzi wa uhusiano wa Kenya na China ambao alisema uliwezesha ujenzi wa miundomsingi muhimu nchini ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR) na barabara ya Nairobi Expressway miongoni mwa mingine.
Mnamo Jumamosi, Rais Ruto alifungua soko la bidhaa za kilimo kutoka Kenya katika nchi hiyo ya Asia.
“Nilifanya mazungumzo na Rais Xi Jinping jijini Beijing, China, kabla ya kongamano la ushirikiano wa Afrika na China. Katika mkutano huo, Rais Xi alikubali mazao ya kilimo kutoka Kenya kuuzwa katika soko la China,” Rais Ruto alitangaza kupitia mitandao ya kijamii.
Katika hali iliyoonekana kumeza chambo cha nchi hiyo, Rais Ruto alisema walikubaliana kujadili miradi ya maendeleo kama vile upanuzi wa SGR na barabara kuu ya Rironi-Mau Summit hadi Malaba.
“Kenya na China zina uhusiano mzuri wa kidiplomasia. Uhusiano huu umekuwa na manufaa ya kirafiki kwa nchi zetu mbili na kubadilisha pakubwa miundomsingi ya reli, barabara na bandari za Kenya,” Rais Ruto alisema.