Ruto alivyoimaliza ODM kupunguza upinzani dhidi ya utawala wake
RAIS William Ruto jana alionekana kumeza ODM na kupunguza upinzani dhidi ya utawala wake baada ya kuwateua vigogo wa chama hicho kwenye baraza lake la mawaziri.
Kiongozi wa nchi jana aliteua uongozi wa juu wa ODM huku ikiwa dhahiri kuwa sasa ana ushirikiano mufti wa kisiasa na kigogo wa chama hicho Raila Odinga.
Naibu kiongozi wa ODM Wycliffe Oparanya jana aliteuliwa waziri mteule wa vyama vya ushirika huku Hassan Joho ambaye pia alikuwa akishikilia wadhifa sawa na huo chamani, akipewa wizara ya Madini.
Mabw Oparanya na Joho walihudumu kama magavana wa ODM katika kaunti za Kakamega na Mombasa mtawalia kati ya 2013-2022.
Rais Ruto pia alimteua Mwenyekiti wa ODM John Mbadi kusimamia wizara ya Fedha.
Kama hayo hatoshi, Opiyo Wandayi ambaye ni Kinara wa Wachache kwenye Bunge la Kitaifa na mbunge wa Ugunja, sasa ni waziri mteule wa Kawi. Bw Wandayi pia ni katibu anayesimamia masuala ya kisiasa ndani chama hicho cha chungwa.
Katika teuzi hizo, ODM ilionekana kupokezwa wizara za hadhi ishara kuwa mazungumzo yamekuwa yakiendelea kati ya Bw Odinga na Rais kuhusu suala la kubuniwa kwa serikali ya muungano.
Wikendi, suala la kubuniwa kwa serikali muungano lilionekana kugawanya ODM kwenye mirengo miwili moja ukimshinikiza Bw Odinga asishirikiane kisiasa na Rais. Mrengo mwingine nao ulionekana ukipinga vikali wanasiasa kutoka chama hicho kujiunga na serikali.
Gavana wa Siaya James Orengo, Seneta wa Nairobi na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna na mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ni kati ya viongozi ambao walikuwa wameonya uongozi wa ODM dhidi ya kushirikiana na Rais Ruto.
“ODM haiwezi kuingia kwenye mtego huo ilhali ni juzi tu Ruto alituita majina na hajaomba msamaha. Kipi kimebadilika mapema hii?” akauliza Bw Orengo kwenye hafla moja ya mazishi Kaunti ya Siaya.
“Katika baadhi ya sehemu za nchi watu bado wanawazika waliouawa wakati wa maandamano lakini viongozi wengine nao wanaweka mikakati ya kujiunga na serikali,” akaongeza.
“Kujiunga na Ruto ni janga. Hatua hiyo ni mwiko kwa sababu serikali hii inaelekea kuporomoka na ni dhahiri kuwa Wakenya wamepoteza imani na Ruto,” akasisitiza.
Hata hivyo, Bw Mbadi, Mbunge wa Homa Bay Mjini Opondo Kaluma na Bw Wandayi ambao walikuwa kwenye mrengo uliopigia upato serikali ya muungano, walisisitiza kuwa hiyo ndiyo ilikuwa njia pekee ya kuleta uwiano nchini.
Bw Kaluma mnamo Jumanne bungeni ,alimkashifu Bw Sifuna ambaye alikuwa ametuma barua ikieleza kuwa ODM haikuwa na nia ya kujiunga na utawala wa Rais Ruto.
“Tunataka kuona yale majina ambayo Baba (Raila) alimtumia Rais yakitangazwa kama mawaziri. Nawaona wengine wanatuma barua eti tukienda serikalini basi tuko kivyetu
“Tulikutana na kuamua tujiunge na serikali kwa sababu ODM ikiongea hata Azimio imezungumza. Tuko katika wakati ambapo taifa linatutegemea kutoka mwelekeo,” akasema Bw Kaluma.
Bw Mbadi naye kwenye mazishi wikendi kule Suba alitofautiana na Bw Orengo ambaye msimamo wake ulikuwa ukionekana kama kizingiti kwa Raila kushirikiana na Rais Ruto.
“Nataka kumwambia Jim (Orengo) kuwa Kalonzo hatupeleki popote na hata Uhuru Kenyatta hana nia njema na sisi kwa sababu alishindwa kutupokeza uongozi mnamo 2022,” akasema Bw Mbadi.
Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati kuna mpango unaendelea wa kuviunganisha ODM, ANC and UDA kuelekea uchaguzi wa 2027.
Aidha aliongeza kuwa ODM itaendelea kuvuna kwa kuwa huenda ikatengewa viti vingi vya makatibu kwenye baraza la mawaziri. Kuhusiana na upinzani nchini, mchanganuzi huyo anasema hilo sasa limebakia Gen Z kwa sababu Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka hataweza kukabili serikali.
“Ukiangalia uteuzi huo, Ruto amepeana wizara zake kwa ODM naye Gachagua amesalia na zile za Mlima Kenya. Upinzani sasa umesalia kuwa wa mwananchi kwa sababu Kalonzo hata akishirikiana na uhuru, hana uzito wowote wa kisiasa kusumbua muungano wa Raila na Ruto,” akasema Bw Andati.
Hii si mara ya kwanza Ruto na Raila wanashirikiana kwa kuwa wawili hao walikuwa ndani ya ODM kwenye uchaguzi wa 2007.