Habari za Kitaifa

Salasya anyoroshwa na mashabiki Nyayo

Na CECIL ODONGO March 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE wa Mumias Mashariki Peter Salasya Jumapili aliona cha mtema kuni na kuokolewa mikononi mwa mashabiki waliojawa na hasira waliomvamia katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo na kumwaangushia kipigo kikali. 

Alikuwa amehudhuria mchuano wa kufuzu Kombe la Dunia 2026 kati ya wenyeji Harambee Stars na Gabon.

Baadhi ya mashabiki walitamka wazi kuwa walikerwa na hatua ya Bw Salasya kuweka video mtandaoni akimkashifu na kumkejeli Kinara wa Upinzani Raila Odinga. Pia walimtaka aheshimu Rais William Ruto ambaye kwa sasa ni mshirika wa Bw Odinga katika serikali jumuishi.

Mbunge huyo mbishi alipachika video hiyo baada ya Raila kupoteza kura ya uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika mwezi uliopita. Jumapili, mashabiki walimpiga vibaya Bw Salasya ndani ya uwanja na hata kumrushia tangi kisha wakamwaandama hadi nje ya uwanja ambako alitoroshwa.

“Heshimu baba, hatukutaki hapa, kwenda huko,” mashabiki hao wakamzomea huku wakimpiga naye Bw Salasya akikimbia lakini bado akalemewa.

“Apigwe kabisa ni mjinga huyo, heshimu baba, heshimu rais,” wakamwakia wakiendelea kumwaangushia kipigo kikali.

Polisi waliokuwa wakimkinga walipata wakati mgumu baada ya kulemewa na ghadhabu za raia huku mbunge huyo akiingizwa kwenye gari na kutoroshwa.

Bw Salasya ambaye alikuwa amevalia jezi ya AFC Leopards hakupata nafasi ya kutazama mchuano huo ambao ulihudhuriwa na halaiki ya mashabiki.

Mwanasiasa huyo alichaguliwa kupitia DAP Kenya inayoegemea mrengo wa Eugene Wamalwa na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya. Mrengo huo ni hasimu kwa ule wa Rais William Ruto na Bw Odinga.

Baada ya Raila kushindwa AUC, Bw Salasya alipinga vikali hatua yake ya kurejea katika siasa za nchi na kusema mara nyingi waziri huyo mkuu wa zamani amekuwa akiangalia maslahi ya tumbo lake.