Urais 2027: Jamii ya Abagusii njiapanda kuhusu Matiang’i na Maraga
JAMII ya Ekegusii imejipata katika njia panda kuhusu ni nani kati ya wana wao wawili inapaswa kuunga mkono katika kinyang’anyiro cha urais 2027.
Je, ni waziri wa zamani Dkt Fred Matiang’i au Jaji Mkuu mstaafu David Maraga?
Japo Dkt Matiang’i hajatangaza rasmi nia yake ya kumng’oa mamlakani Rais William Ruto, wanaomuunga mkono kwa wadhifa huo wako mbioni kote nchini wakimpigia debe.
Hali hiyo imechangia kupanda kwa joto la siasa nchini.
Kwa upande wake, Jaji Maraga ameanza kuzuru maeneo mbalimbali nchini kukadiria hali kabla ya kuanzisha kampeni rasmi ya urais.
Wikendi iliyopita, alikumbana na kundi la watu walioonekana kupinga ndoto yake katika Kaunti ya Nyamira anakotoka sawa na Dkt Matiang’i.
“Je, ni Matiang’i au Maraga?” diwani wa Wadi ya Rigoma Nyambega Gisesa akauliza kwa sauti ya juu.
Umati ukajibu kwa pamoja, “Matiang’i!” Huku akijibu umati huo, Maraga alisema kwa lugha ya Ekegusii, “Sikuja hapa kumtusi au kumdhalilisha mtu yeyote. Hayo ni masuala ambayo yatajadiliwa wakati unaofaa baada ya hali kutulia.”
Lakini Bw Gisesa aliwataka wakazi wasikanganyike kuhusiana na wawili hao.
“Tunawataka nyie watu wetu kumuunga mkono Matiang’i na tuheshimu viongozi,” akasema huku akishauri hadhira kutofautisha kati ya Dkt Matiang’i na Bw Maraga.
“Nani anawania urais? Matiang’i au Maraga?” akauliza Bw Gisesa, huku wengi wakijibu “Matiang’i”.
Baadhi ya watu katika umati huo, hata hivyo, walimshauri Bw Maraga awanie wadhifa wa Gavana wa Nyamira.
Jaji Mkuu huyo mstaafu alisema kuwa watu wengi ambao ametangamana nao wanalalamikia huduma mbovu inayotolewa na serikali, changamoto ambayo alisema inapasa kushughulikiwa.
“Nimekuwepo kwa siku kadhaa na watu wanalilia huduma. Wanawataka viongozi (katika Bunge la Nyamira) kuketi na kusuluhisha tofauti zao,” akasema Bw Maraga.
Jaji Maraga aliandikisha historia mnamo 2017 kwa kuongoza Mahakama ya Juu kufutilia mbali ushindi wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta dhidi ya kiongozi wa ODM Raila Odinga. Kwa upande mwingine, utendakazi wa Matiang’i katika wizara mbalimbali ulimpa sifa kama afisa wa serikali anayelenga kuleta mageuzi katika sekta ya umma.
Kwa mfano, aliimarisha viwango vya elimu kwa kupambana vikali na visa vya udanganyifu katika mitihani ya kitaifa. Alifanya hivyo kwa kujituma na kutembelea shule mbalimbali nchini, hali iliyomfanya aonekane kama waziri aliyejitolea kwa kazi yake.
Utendakazi wa Dkt Matiang’i na Bw Maraga ulishabikiwa na idadi kubwa ya Wakenya, hali ambayo itavutia idadi kubwa ya wapigakura kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Kinachovutia na kuonekana kama sadfa ni kwamba wawili hao wanatoka Kaunti ya Nyamira na ni waumini wa Kanisa la Kiadventista (SDA).
Dkt Matiang’i na Maraga ni viongozi waadilifu na wamejitolea kutokomeza jinamizi la ufisadi, kurejesha nidhamu katika utumishi wa umma, uwajibikaji na utawala wa sheria.