Viongozi wa walimu waenda Ikulu kumsihi Ruto awaangalilie mambo ya posho
MAAFISA wa Chama cha walimu wa shule za sekondari na vyuo (Kuppet) waliokutana na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi mnamo Jumamosi waliomba awasaidie kuimarisha mazingira yao ya kazi na pia waongezwemishahara na marupurupu.
Katika mkutano huo wa mwisho wa wiki, Kuppet iliongozwa na Mwenyekiti Omboko Milemba na Katibu Mkuu Akello Misori.
Haya yanajiri baada ya Kuppet kulalamika kuwa Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC), haijakuwa ikiwasilisha makato ya wanachama kwa muungano huo kwa kipindi cha miezi mitatu.
Kupitia taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo, Bw Misori alidokeza kuwa chama hicho kilimweleza Rais kuhusu maslahi na hali ya mazingira ya kazi ya walimu.
“Kuppet iliomba Rais ahakikishe kuwa TSC inapata fedha zaidi ili kuwapandisha walimu 130,000 vyeo, kuajiri walimu zaidi na kutathmini marupurupu mbalimbali ya walimu,” alisema Bw Misori.
Dkt Ruto alieleza kuwa TSC wakati mwingine haiwezi kutatua changamoto za walimu kwa mfano kuhusu kutengwa kwa fedha ili kuwaajiri walimu.
“Katika masuala haya, Rais alituomba kukumbatia mazungumzo na serikali hadi afisi ya urais, na mgomo uwe uamuzi wa mwisho,” aliendelea Bw Misori.
Vile vile, Rais alitaka wanachama wa Kuppet kuendelea kusaidia miradi ya serikali kama vile mradi wa nyumba za gharama nafuu huku chama hicho kikiangazia njia tofauti kuhakikisha walimu wananufaika na mpango huo.
Suala la tata la TSC kukosa kuwasilisha makato ya uanachama halikuangaziwa – kulingana na taarifa ya Kuppet baada ya mkutano na Rais.
Fedha hizi husaidia vyama vya wafanyakazi kuendeleza shughuli zao za kila siku kutetea maslahi ya wanachama.
Uongozi wa matawi ya Kuppet katika kaunti 47 kote nchini umelalamikia hali ya ukosefu wa fedha.
Hali imekuwa mbaya kiasi cha maafisa wa Kuppet katika Kaunti za Kisumu, Homa Bay na Nairobi kuomba msaada kutoka kwa walimu, wanasiasa na makundi ya mtandao wa kijamii wa Whatsapp ili wapate pesa za kuendeleza baadhi ya shughuli za chama.
Mjini Nairobi, maafisa wa tawi la jiji kuu wamedai kuzongwa na mikopo baada ya kushindwa kuilipa.
Kulingana na Katibu Mtendaji Moses Bomara, hatua ya TSC kukosa kuwasilisha makato imewataabisha wanachama.
“Kuteseka huku kumetosha. Mali yetu inatwaliwa na benki zilizotukabidhi mikopo. Hatuna uwezo wa kulipa kodi ya nyumba na wafanyakazi. Kinachofanyika sasa si haki na ni kinyume cha sheria,” alisema Bw Bomara.
Matatizo sawa yanashuhudiwa katika kaunti nyingine nchini ambapo maafisa wa vyama wanalazimika kukopa kutoka kwa wanachama ili shughuli za vyama ziendelee.