Waandamanaji 11 wafidiwa Sh2.2 milioni kwa kudhulumiwa na polisi
WAANDAMANAJI 11 wamefidiwa Sh 200, 000 kila mmoja na Mahakama Kuu baada ya polisi kukiuka haki zao wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024.
Aidha, mahakama imeamua kuwa maafisa wa polisi wanaopelekwa kudumisha usalama wakati wa mikutano ya hadhara, maandamano au migomo lazima wavalie sare na wasifiche nyuso zao.
“Afisa yeyote anayeteuliwa kuhakikisha sheria na utulivu wakati wa mkutano wa hadhara, maandamano au migomo lazima awe kwenye sare rasmi, na asifiche uso wake kwa njia yoyote ile ili aweze kutambulika,” alisema Jaji Bahati Mwamuye.
Mahakama iliagiza Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja kuhakikisha kuwa maafisa wote waliotumwa kudhibiti maandamano au kutoa ulinzi kwa waandamanaji hawavai mavazi ya kiraia au kuvaa barakoa.
Maamuzi haya yalitokana na kesi ya Chama cha Wanasheria Kenya (LSK) dhidi ya maafisa wawili wa polisi, Martin Mbae Kithinji na Isaiah Ndumba Murangiri, waliokuwa miongoni mwa waliotumwa kudhibiti maandamano ya Juni 2024.
LSK ilidai kuwa Bw Murangiri ndiye aliyehusika na kifo cha Rex Masai, mmoja wa waandamanaji aliyeripotiwa kupigwa risasi na polisi Juni 18, 2024 katika jiji la Nairobi wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha.
Kulingana na LSK, visa vyote vya mauaji, ukatili wa polisi na unyanyasaji wa waandamanaji vinahusishwa na maafisa wasiovalia sare rasmi.
Mahakama ilisema kuwa kuvaa mavazi ya kiraia kuliwasaidia maafisa wa polisi kujichanganya na waandamanaji waliokuwa na amani.
Serikali iliagizwa kuwalipa waandamanaji — Joy Awich, Muthoni Matu, Kipng’etich Eman, Carolyne Mwikali, Stephen Obunde, Raymond Burgei, Felix Gatobu, Chatherine Njoki Njanja, Tim Kut, Wesley Tome na Imran Kasumba — jumla ya Sh2.2 milioni.