Habari za Kitaifa

Wanjigi adai serikali ya Ruto inatishia kumwangamiza

Na DANIEL OGETTA, MWANGI MUIRURI August 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

MFANYABIASHARA Jimi Wanjigi sasa anadai kwamba serikali ya Rais William Ruto inataka kumwangamiza, siku kadhaa baada ya kumthubutu Kiongozi wa Nchi amchukulie hatua kwa kufadhili maandamano dhidi ya serikali; kitendo anachosema si uhalifu.

Bw Wanjigi, 61, amekuwa akitofautiana na serikali mbili zilizopita za Kenya: serikali ya Jubilee ya Rais Uhuru Kenyatta ambayo aliisaidia kuingia mamlakani mwaka wa 2013 na sasa utawala wa Kenya Kwanza wa Dkt Ruto.

Katika mahojiano na Runinga ya moja Jumanne usiku, Bw Wanjigi alisema masaibu yake na tawala hizi mbili yanatokana na makubaliano ya 2009 kati yake, Bw Kenyatta na Dkt Ruto.

“Wakati huo, Uhuru Kenyatta na Ruto walinijia, wakikabiliwa na kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) iliyotokana na ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/8 ambazo zilisababisha vifo vya watu zaidi ya 1,100, maelfu ya watu kuhama makazi yao na kuwaacha wengine wakiwa vilema,” alisema.

“Walikuja kwangu niwasaidie kupanga njia ya kuingia madarakani kwa lengo la kutumia nguvu za wananchi ili wajivue minyororo ya kesi. Waliogopa kufungwa jela, kupoteza walichokuwa nacho na aibu.”

Alisema kwamba alikubali na wakaafikiana kwamba “baada ya mimi kuwaokoa, lazima waokoe nchi kwa kubuni mbinu mpya za kufanya mambo”.

Baada ya kushinda, alisema, walikiuka makubaliano na kuanza kuzingatia maslahi yao ya kibinafsi.

Alisema kuwa alipowashinikiza kuheshimu makubaliano hayo, “walinichapisha katika kurasa za wafu kama njia ya kunipa ahadi ya kifo”.

Kinara wa Upinzani Raila Odinga (katikati) akiwa na mfanyabiashara Jimi Wanjigi (kulia) katika hafla ya awali Kajiado. Picha|Maktaba

“Nilipoanza kumuunga mkono Odinga (uchaguzi wa 2017) walijua ni nani anaweza kuwaondoa madarakani na dhiki zangu  zikaanza. Sasa zimeongezeka wakati wa  Rais Ruto kiasi kwamba mimi na familia yangu tunavamiwa na kufungiwa katika nyumba yangu”.

Serikali zote mbili za Dkt Ruto na Bw Kenyatta bado hazijafaulu  kumkamata katika nyumba yake ya kifahari mtaani Muthaiga.

Wiki iliyopita, polisi walipiga kambi katika nyumba hiyo kwa zaidi ya saa 24, wakimsaka kiongozi huyo wa chama cha Safina bila mafanikio—walifanikiwa kuwakamata baadhi ya wafanyakazi wake ambao sasa wanakabiliwa na mashtaka ya kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Wanjigi alipata agizo la mahakama kuzuia polisi kumkamata. Hata hivyo, anashikilia kuwa yaliyotokea wakati wa Bw Kenyatta na sasa Dkt Ruto, ni ” uhalifu” unaonuiwa kumpeleka kaburini.

“Nadhani ni mimi wanayetafuta. Katika matukio yote mawili, imekuwa ni mimi wanayetaka,” Bw Wanjigi alisema.

Asema madai ya kuweko silaha kwake ni hadaa tu ya serikali

“Kwa nini waje na kusema nina guruneti?” alisema na kueleza kuwa “kusema nina guruneti ni kusema kwamba ninapigana na nchi hii kwa kutumia silaha. Nimekuwa nikizungumza [kuhusu] jambo moja tu—uchumi.”

Katika matukio hayo mawili, alieleza, “walileta bunduki” nyumbani kwake.

“Sasa wanasema nilikuwa na mabomu, guruneti, vitoza machozi na kadhalika.”

Alipoulizwa kwa nini serikali mbili tofauti zizozane na mtu mmoja, alijibu: “Ni wao wananiogopa. Hii haijawahi kutokea kwa mtu mwingine yeyote chini ya tawala hizo.”

Familia yake ya karibu – mke wake, watoto na mama yake – walitazama na kuingiwa na hofu polisi walipokuwa wakimsaka mtu ambaye serikali inaamini kuwa amekuwa akifadhili maandamano ya vijana.

Jamaa zake, alisema, walikuwa jasiri sana na walistahimili shinikizo hizo.

“Hata waliotaka nijitokeze walikuwa wananiambia hapana. Watu hawa wakikukamata, watakuua. Hawatatuua sisi. Wanaweza kututishia tu na labda watutie ndani. Lakini itakuwa vigumu kutuua”.

Mwishoni mwa juma, polisi walivamia nyumba ya Bw Wanjigi na kuchukua baadhi ya mali yake katika operesheni ambayo wanasiasa wa upinzani Martha Karua na Kalonzo Musyoka waliitaja kuwa hujuma.

Baada ya kupata agizo la korti, mfanyabiashara huyo aliibuka tena kutoka  katika maficho yake na kuwakejeli polisi kwa kupoteza wakati.

Katika uvamizi  wa 2017, kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga alilala nyumbani kwa Bw Wanjigi na kulazimu polisi kuacha msako wa kumkamata mfanyabiashara huyo. Bw Odinga na Bw Wanjigi, wakati huo, walikuwa upande mmoja wa kisiasa.

Bw Wanjigi alieleza kuwa hakuzungumza na Bw Odinga alipofika nyumbani kwake, kwa sababu familia yake ilihisi kuwa haikuwa salama.

Kinara huyo wa upinzani amekuwa mshirika wa Rais Ruto,  ushirika ambao umefanya baadhi ya viongozi wa chama chake kujiunga na serikali, katika kile kinachoitwa Serikali Jumuishi.

Mnamo Jumanne, Bw Odinga alidai kuwa Bw Kenyatta, ambaye alifanya kampeni dhidi ya Dkt Ruto katika uchaguzi wa 2022, aliwasiliana naye ili kuokoa nchi baada ya ghasia za vijana ambazo hazijawahi kushuhudiwa.

Lakini muungano huo mpya na unavyotetewa, Bw Wanjigi alisema, “si wa kawaida.”

Alisema kuwa duniani kote, kila kunapokuwa na machafuko ya wananchi, jambo la kwanza ambalo serikali iliyo mamlamkani hufanya “ni kuunda serikali ya umoja” kwa kuwaleta pamoja  viongozi wote wa kisiasa.

“Rais William Ruto anataka kila mtu awe katika serikali yake inayozama ili raia wasiwe na sauti mbadala. Amealika watu kwenye serikali inayozama,” akasema Bw Wanjigi.

“Tulikuwa tayari tumeungana na tuliunganishwa na maumivu ya kiuchumi. Bado tumeungana katika maumivu hayo ya kiuchumi. Wanaweza kufanya yote wanayotaka huko juu lakini ninakuhakikishia, wako kwenye meli inayozama na Wakenya hawatajiunga nao. Watazama wenyewe.”

Alishangaa kwa nini rafiki yake Bw Odinga alikuwa na miguu yote miwili kila mahali, akidai kuwa nje ya serikali huku matukio ya hivi punde yakionyesha kingine — kwamba yuko serikalini.