Habari za Kitaifa

Wazazi wa majenzii waliouawa katika maandamano wataka watoto wao watambuliwe Mashujaa Dei

Na DANIEL OGETTA October 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

AKINA mama waliopoteza watoto wao wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024, wanaomba watoto wao waenziwe Siku ya Mashujaa Dei Oktoba 20, 2024.

Akina mama hao wanadai kuwa vifo vya wanao vilileta mabadiliko makubwa nchini.

Mamake Kenneth Njeru, Kelvin Odhiambo na Erickson Kyallo katika barua ya wazi ya kuhuzunisha walieleza huzuni yao wakisema wanao wanafaa kukumbukwa siku hiyo.

Wana wao, kama wengine wengi, walikuwa baadhi ya vijana waliouawa wakati wa maandamano ya kihistoria nchini.

“Mwanangu aliona jinsi nilivyofanya kazi kwa bidii, mchana na usiku na katika miaka yake ya ishirini, akaamua kunipigania. Wakenya wenzangu, tunapoadhimisha Siku ya Mashujaa, tuikite siku hii mioyoni na akilini mwetu. Tudai mnara wa kuwakumbuka hawa mashujaa waliopigania Katiba iheshimiwe. Hii lazima iwe sababu ya sisi kukusanyika kila mwaka katika Siku ya Mashujaa – kuheshimu ujasiri wao na kujikumbusha kuwa tutaendelea kupigania haki yetu.”

“Maandamano, kwa vijana kama Kenneth, Kelvin, na Erickson, hayakuwa tu kuhusu siasa – yalikuwa kuhusu haki.Walifanya kitu ambacho hakijawahi kutokea; hatujawahi kuona,” akina mama waliandika, wakikumbuka maono ya nguvu ya watoto wao wakitaka mabadiliko nje ya Bunge.

“Milio ya risasi ilianza, na tuliona vijana wakianguka moja baada ya mwingine na kumwaga damu barabarani,” wanasimulia waziwazi vurugu zilizozuka.

Lakini barua ya wazi ni zaidi ya kusimulia tu hasara ya kibinafsi; ni kilio cha haki.

Akina mama hao wanakumbuka siku za kutisha ambapo watu walitoweka bila kujulikana, kutekwa nyara na vikosi vya wahuni kuiba bila kuwajibishwa.

“Hatukuwaza kamwe kwamba macho yetu yangeshuhudia mambo kama haya,” wanaandika.

“Nilitarajia kwamba katiba ingemlinda mtoto wangu, ili asiwahi kuishi katika enzi ya mateso, hofu ya kujieleza, kukusanyika au kuandamana.”

Lakini kama barua hiyo inavyoonyesha kwa uchungu, mili ya watoto wao ilipelekwa katika vyumba vya kuhifadhia maiti, baadhi ikiwa imekatakatwa.

“Hadi sasa, hatujapata mtu yeyote anayetuambia ni nani aliyefanya hivi, na hakuna mtu anayewajibika,” mama huyo alisema.

Mashirika ya haki za binadamu yalisema vifo vilivyotokana na maandamano ya kuipinga serikali vilikuwa 50 kufikia Juni 2024.

“Pesa haziwezi kamwe kurudisha uhai,” akina mama hao waliandika.

“Kinachowaumiza moyo zaidi ni kuwa serikali ya Rais William Ruto haijaonyesha dalili yoyote ya kujali. Wanarejelea vifo vya kusikitisha vya watoto katika shule ya Hillside Endarasha Academy, ambapo 21 walikufa kutokana na moto ulioteketeza bweni la wavulana katika taasisi hiyo. Cha kushangaza ni kuwa hata baada ya vifo hivyo kutokea, shule hiyo bado inafunguliwa tu.”