HabariSiasa

Hofu mpya kuhusu madeni ya Uchina

January 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LEONARD ONYANGO

SERIKALI Jumatatu ilikaa kimya kuhusu taarifa kuwa imepatia China uhuru wa kutwaa mali ya Kenya ipendavyo iwapo itashindwa kulipa deni la mabilioni ya fedha za ujenzi wa reli ya kisasa, SGR kutoka Mombasa hadi Nairobi.

Juhudi za kupata Serikali kuweka wazi suala hilo Jumatatu hazikufua dafu kwani maafisa wa Serikali hawakutaka kuzungumzia suala hilo, ambalo limezua taharuki miongoni mwa maafisa wakuu tangu Jumapili habari hizo zilipofichuka.

Taifa Leo ilifahamu kuwa maafisa husika walikuwa kwenye mikutano mchana kutwa jana katika jitihada za kutafuta mbinu za kukabiliana na habari hizo ambazo zimewatia Wakenya hofu ya mali na uhuru wa nchi yao kutwaliwa na China.

Ili kufichua kipengele chochote cha mkataba huo, serikali ya Kenya ilifaa kupata ruhusa kutoka China kwa njia ya maandishi.

Ni kifungu hiki ambacho kimezua hali ya wasiwasi miongoni mwa maafisa wa serikali baada ya kufichuka kwa yaliyomo ndani ya mkataba huo uliotiwa saini na Waziri wa Fedha Henry Rotich na Bw Li Riogu ambaye alikuwa mwenyekiti wa Benki ya Exim ya China wakati huo.

Ujenzi wa reli ya SGR kutoka Mombasa hadi Nairobi uligharimu Sh327 bilioni. Mkondo wa pili wa ujenzi wa reli hiyo kutoka Nairobi hadi Naivasha utagharimu Sh160 bilioni kulingana na mkataba uliotiwa saini kati ya Kenya na Benki ya Exim.

Ujenzi wa awamu ya mwisho wa reli kutoka Naivasha hadi mpaka wa Malaba unatarajiwa kugharimu Sh500 bilioni.

Mwaka huu, wizara ya Fedha italipa Sh56.7 bilioni kwa Benki ya Exim, kulingana na makadirio ya bajeti.

Habari hizo zimechipuka wiki chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukanusha kwenye mahojiano ya moja kwa moja na wanahabari kuwa Serikali iliweka sahihi mkataba ambao unakubalia China kutwaa usimamizi wa bandari ya Mombasa iwapo itashindwa kulipa deni hilo.

Lakini sasa imefichuka kuwa sio tu bandari inayoweza kutwaliwa na Wachina, mbali wako huru kutwaa mali yoyote ndani na nje ya nchi kwa mujibu wa mkataba uliowekwa sahihi Mei 11, 2014.

Mkataba huo unafichua nia kuu ya China kutwaa mali ya Kenya kwani katika mkataba huo inasema inaweza kukataa malipo ya deni hilo iwapo Kenya itapata pesa kwa njia nyingine isipokuwa ile imekubalika chini ya mkataba huo.

“Benki ya China ya Exim iko na uhuru wa kukataa malipo ya Kenya yakilipwa kitita iwapo yatatoka kwingine, ama inaweza kutoa masharti kabla ya kukubali na pia inafaa kujulishwa kabla,” mkataba huo unadokeza.

Makubaliano hayo ambayo yananyanyasa Kenya pia yana kipengee ambacho kinasema sharti Kenya iagize bidhaa, tekinolojia na huduma kutoka China. Hili limedhihirika kufuatia kufurika kwa bidhaa za China nchini zikiwemo bidhaa zinazopatikana nchini kama samaki.

“Mzozo unaotokana na mkopo huo utaamliwa na Tume ya Kutatua Mizozo ya Kiuchumi na Biashara ya Kimataifa ya China (CIETAC). Uamuzi utakaotolewa na CIETAC utakuwa wa mwisho,” kinasema kipengee cha 8.5 cha mkataba huo.