Habari

Iko kazi! TSC yatangaza zaidi ya nafasi 9,000 za kazi

Na MERCY SIMIYU November 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TUME ya Kuwaajiri Walimu Nchini (TSC) imetangaza nafasi 9,159 za ualimu ili kuziba pengo la waliostaafu, kujiuzulu na walioaga dunia.

Hatua hii itakuwa nafuu kwa shule ambazo zimekuwa zikikabiliwa na uhaba wa walimu.

Kwenye notisi ambayo Taifa Leo Dijitali imefaulu kuiona, TSC imesema kuwa nafasi zote zitajazwa ambapo walimu 7,056 watakuwa wa shule za msingi.

Pia walimu 2,082 watakuwa shule za upili huku 12 wakiwa wa kufundisha katika Shule za Sekondari za Chini (JSS).

“Wanaotaka kazi hii wawasilishe stakabadhi zao kupitia tovuti ya TSC kabla ya saa sita usiku wa Disemba 8. Maelezo kuhusu nafasi hizi za ajira ziko kwenye mtandao wa TSC,” notisi hiyo ikasoma.

Tangazo hili limetolewa wakati ambapo kuna mianya ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara katika taaluma ya elimu.

Mnamo Disemba 2024, TSC ilitangaza kuwa kulikuwa na nafasi wazi 8,707 kutokana na sababu mbalimbali ilhali takwimu kutoka Juni 2022 hadi Januari 2023 zilionyesha kuwa kulikuwa na nafasi 8,018.

Hivi majuzi ripoti zilionyesha kuwa kulikuwa na nafasi 2,014 mnamo Mei 2025. Walimu 10,245 wanatarajiwa kuondoka kwenye taaluma ya ualimu kufikia Juni 2025.

Kwa mujibu wa TSC, uajiri wa walimu unalenga kuhakikisha kuwa shule haziathiriki baada ya walimu kustaafu, wengine kujiuzulu na baadhi kufa.

Aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Nancy Macharia, awali alikuwa ameonya kwamba upungufu huo ni hatari huku shule za sekondari ya chini na za juu zikiwa na upungufu wa walimu 98,261 Alionya kuwa pengo litakuwa kubwa zaidi hasa wanafunzi wakijiunga na gredi ya tisa mnamo 2026, hali hiyo ikilemaza utekelezaji wa Mtaala wa Ubunifu na Utendaji (CBC).

“Tunahitaji Sh5 bilioni kila mwaka kuwapandisha walimu ngazi na kuhakikisha kuwa wanaendelea kwenye taaluma yao. Tuna zaidi ya walimu 300,000 ambao hawajaajiriwa kwenye sajili yetu.

“Hoja kuu ni kwenye bajeti ambapo sisi hupokea Sh1 bilioni ambayo inawaajiri walimu 6,000 pekee,” akasema alipofika mbele ya kamati ya bunge kuhusu elimu.

Kando na nafasi zilizotangazwa, TSC pia inalenga kuwaajiri walimu wakufunzi 24,000 mnamo Januari 2026 kupunguza uhaba ambao umekwepo katika shule za msingi na sekondari.

Haya yanakuja huku mkataba wa walimu wakufunzi 20,000 ukitarajiwa kutamatika mnamo Disemba.