Kijana aliyetoroka Al Shabaab asimulia maisha yalivyokuwa akiwa gaidi
Na MOHAMED AHMED
Kwa Muhtasari:
- Kijana huyo amekuwa akiishi maisha ya kisiri ili maafisa wa usalama ama wafuasi wa Al Shabaab wasimtambue
- “Nilimtembelea binamu yangu Lamu na kuishi kwake kwa miezi mitatu. Baadaye alinijulisha kwa vijana wengine watatu kisha akatupa Sh10,000 kila mmoja”
- “Tulifika kwenye kambi iliyokuwa na vijana wapatao 200. Hapo ndipo nilipong’amua kuwa nilikuwa ndani ya kambi ya Al Shabaab nchini Somalia”
- Mafunzo yalihusisha jinsi ya kutumia silaha tofauti kama bunduki, gurunedi miongoni mwa nyingine. Pia tulibebeshwa magunia mazito yaliyojaa mchanga
- “Singeweza kuvumilia tena. Mwezi moja baada ya kugombana na kamanda, nilipanga na Mkenya mwingine jinsi tungehepa”
VIJANA wanaorudi nchini baada ya kuhepa Al Shabaab nchini Somalia wanajutia kwa kujiunga na kundi hilo la kigaidi.
Majuto yao yanatokana na kuwa hawawezi kuishi maisha ya kawaida kwa hofu ya kuwindwa na polisi ama kuuawa na wafuasi sugu wa kundi hilo ambalo limetatiza usalama hasa kaunti za Lamu, Wajir na Mandera.
Taifa Leo ilikutana na mmoja wa vijana hao, ambaye ni kijana wa miaka 29 katika kaunti ya Kwale aliyerudi nchini 2015.
Kijana huyo amekuwa akiishi maisha ya kisiri ili maafisa wa usalama ama wafuasi wa Al Shabaab wasimtambue. Tulipomtembelea nyumbani kwao, mwanzo alikataa kuzungumza nasi kwa kuhofia kuwa tulikwa makachero. Lakini alikubali tulipomhakikishia kuwa sisi ni wanahabari:
“Safari yangu ya kujiunga na Al Shabaab ilianza 2014. Binamu yangu alinialika Lamu kwa ahadi kuwa ningepata kazi nzuri. Alifahamu kuwa nilikuwa nafanya vibarua hapa na pale licha ya kuhitimu katika Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS). Aliniambia ningeajiriwa kazi yenye malipo mazuri.
Nilimtembelea binamu yangu Lamu na kuishi kwake kwa miezi mitatu. Baadaye alinijulisha kwa vijana wengine watatu kisha akatupa Sh10,000 kila mmoja. Alitwambia tuingie gari la kibinafsi tupelekwe mahala ambapo tungeanza kufanya kazi aliyokuwa ameahidi ambapo tungelipwa Sh40,000 kwa mwezi.
Mafunzo ya miaka miwili
Tulifika kwenye kambi iliyokuwa na vijana wapatao 200. Hapo ndipo nilipong’amua kuwa nilikuwa ndani ya kambi ya Al Shabaab nchini Somalia. Humo kambini tulianza kupokea mafunzo ya kijeshi ambayo yalikuwa yachukue miaka miwili. Baadaye tungetumwa uwanja wa vita kupigana.
Mafunzo yalikuwa makali sana. Tulikuwa tukiamka saa kumi alfajiri ambapo tulishiriki mafunzo na mazoezi hadi saa kumi na moja jioni.
Mafunzo yalihusisha jinsi ya kutumia silaha tofauti kama bunduki, gurunedi miongoni mwa nyingine. Pia tulibebeshwa magunia mazito yaliyojaa mchanga. Ilikuwa ni lazima ushiriki mafunzo upende usipende.
Siku moja kamanda aliniagiza ninyanyue gunia la kilo 50 la mchanga lakini nikateta. Alichomoa kisu kwa nia ya kunidunga. Nilishika kisu hicho kikanijeruhi mkono wa kushoto. Hivyo ndivyo nilivyopata jereha hili mkononi ambalo hunikumbusha masaibu niliyopitia mikononi mwa Al Shaabab.”
Alivyohepa
“Singeweza kuvumilia tena. Mwezi mmoja baada ya kugombana na kamanda, nilipanga na Mkenya mwingine jinsi tungehepa. Ilikuwa Agosti, 2015 ambapo tulitoroka usiku na kuanza kutembea tukiwa na imani tungefika Kenya.
Tulifahamu kuwa hatua hiyo ilikuwa hatari kwani tungeweza kuuawa na wenzetu wa Al Shabaab ama maafisa wa usalama. Lakini tuliamua heri tufe tukitafuta uhuru wetu badala ya maisha ndani ya Al Shabaab.
Baada ya kutembea kwa siku mbili msituni tulipatana na mzee ambaye alitusaidia kufika Mandera. Kisha tuliingia lori lililotupeleka Garissa. Mjini Garissa tulipanda basi lililotupeleka Mombasa kisha mimi nikaja hapa nyumbani naye mwenzangu akaenda kwao Kilifi.
Watu hapa kijijini hawashuku hata kidogo kuwa nilikuwa nimejiunga na Al Shabaab. Niliingizwa katika kundi hilo bila kufahamu. Tangu niliporudi nimekuwa nikiishi maisha ya utulivu na familia yangu. Kinyume na wengine wanaorudi, mimi sitaki kujiingiza katika uhalifu.”