Kimataifa

Israeli yashambulia kambi za jeshi la Iran na Syria ikidai waliichokoza

February 11th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Wanajeshi wa Israeli kaskazini mwa taifa hilo eneo la Alonei Abba, Februari 11, 2018 wakikagua mabaki ya ndege waliyodungua. Picha/AFP

Na AFP

JERUSALEM, ISRAELI

ISRAELI Jumamosi ilishambulia vituo vya Iran nchini Syria baada ya ndege yake ya kivita kuangushwa na jeshi la angani la Syria. 

Kutokana na makabiliano kati ya mahasimu wa jadi Israeli na Iran tangu vita vianze Syria 2011, Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu aliapa kuzuia Iran kuzua msukosuko wa kijeshi katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Mashambulio ya Israeli yalijiri baada ya kunasa ilichotaja kama ndege ya Iran isiyoendeshwa na rubani ikielekea Syria na kusema lilikuwa shambulio.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Israeli kutangaza hadharani kulenga inachotambua kama vituo vya Iran nchini Syria tangu mzozo huo ulipoanza.

Iran ilitaja madai ya Israeli kama uongo na kusema Syria ina haki ya kujilinda ikishambuliwa.

Aidha, Iran pamoja na mataifa mengine inayoshirikiana nayo nchini Syria – Urusi na kundi la Hezbollah lenye makao Lebanon-walikanusha madai ya Israeli kuhusu kunaswa kwa ndege.

Wizara ya mashauri ya nchi za kigeni ya Urusi ilitaka pande zote kuwa na uvumilivu na kusema haikubaliki kuzua vitisho kwa maisha na usalama wa wanajeshi wa Urusi walio Syria.

Msemaji wa jeshi la Israeli, Jonathan Conricus, alionya Syria na Iran kwamba zinacheza na moto, lakini akasisitiza kuwa nchi yake haitaki kuzidisha vita.

“Huu ndio ukiukaji wa hali ya juu wa utukufu wa Israeli kutendwa na Iran katika miaka ya hivi karibuni,” Conricus aliambia wanahabari.

Israeli ilisema ilitekeleza mashambulio makubwa dhidi ya vituo vya jeshi la angani la Syria na vituo vya kijeshi vya Iran.

Wanajeshi wawili wa ndege ya kivita aina ya F16 iliyoangushwa walikuwa hai ingawa mmoja wao alipata majeraha mabaya, jeshi lilisema. Walitua Israeli na kupelekwa hospitalini.

Israeli ilisema makabiliano yalianza baada ya ndege ya kivita isiyoendeshwa na rubani kuingia katika anga yake na kunaswa na helikopta.

Conricus alisema ilinaswa ikiwa ndani ya Israeli kaskazini ya jiji la  Beit Shean, karibu na mpaka wa Jordan.

Hata hivyo, hakueleza ikiwa ndege hiyo ilikuwa na silaha lakini akadai ilikuwa katika shughuli za kijeshi na ilitumwa na wanajeshi wa Iran kutoka kambi ya kijeshi ya Iran iliyoko eneo la Palmyra.

Alisema ndege nane za kivita za Israeli zililenga vituo vya kijeshi vya Iran vilivyoko Syria.

Shirika la haki za binadamu la Syrian Observatory for Human Rights, lenye makao Uingereza, lilisema Israeli ililenga vituo kadhaa vilivyoko mkoa wa kati wa Homs. Shirika hilo lilisema vituo hivyo hutumiwa na Iran na Urusi.

Msemaji wa mashauri ya nchi za kigeni wa Iran Bahram Ghasemi alilaumu Israeli kwa kudanganya akisema Iran haina wanajeshi Syria.