Kimataifa

Juhudi za kufua panga kuwa majembe barani Afrika

November 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KEN WALIBORA akiwa Addis Ababa, Ethiopia

KENYA imejitolea mhanga kuwa mstari wa mbele katika kutokomeza vita na silaha barani Afrika kuambatana na mkakati wa Muungano wa Afrika wa kutokomeza silaha yaani Silencing the Guns.

Mwakilishi wa Kenya katika bunge la Afrika Bi Janet Ong’era alisema kwamba wizi wa kura na kuingiza ukabila katika michakato ya kisiasa pamoja na uteuzi kombo wa viongozi katika nyadhifa mbalimbali ni chanzo cha vita ambavyo Kenya imekuwa ikikumbana navyo mara kwa mara hasa nyakati za uchaguzi mkuu.

Hata hivyo, Bi Ongera alisema kwamba maridhiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na hasimu wake mkuu, Raila Odinga, yamesaidia kupunguza joto la kisiasa na kuleta amani.

Alisema kilele cha ushirikiano huo ni mpango wa kujenga maridhiano (BBI) ambao ulijadiliwa na kuzinduliwa hivi karibuni katika ukumbi wa Bomas of Kenya.

Bunge la Afrika limeshapitisha azimio kunyamazisha bunduki kufikia mwaka ujao 2020.

 

Picha za baadhi ya wajumbe wa bunge la Afrika Novemba 28, 2019. Picha/ Ken Walibora

Wabunge wa bunge la Afrika walikutana katika jiji kuu la Ethiopia, Addis Ababa kujadili mikakati ya kutokomeza vita na silaha barani kuambatana na azimio hilo.

Wabunge hao, ambapo asilimia 90 yao ni wanawake, wamepongeza mikakati ya kutokomeza vita barani lakini wakaonya kwamba pana pengo kubwa kati ya utamkaji wa maazimio na utekekezaji.

Kiranja wa Bunge la Afrika Kusini na ambaye pia ni mbunge wa bunge la Afrika, Pemmy Majodina alisema kwamba vita vitakwisha tu barani Afrika pakiwepo na nia ya kisiasa na vilevile kudhibiti barabara mipaka ambapo silaha hupitishwa kimagendo.

Mbunge wa Uganda Anifa Kawooya, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa kundi la wabunge wanawake barani Afrika, aliwashutumu viongozi wa Kiafrika kwa kuwa wanafiki wakubwa na hivyo kukwamisha upatikanaji wa amani kamili.

Bi Kawooya alisema viongozi wa Afrika wana mazoea ya kutoa matamko ya amani na kutia sahihi mikataba, ilhali bado wanaongeza matumizi ya bajeti ya taifa katika kipengee cha ulinzi na ununuzi wa silaha kalikali.

Alisema ndoto ya kuzizima bunduki barani, haitatimia viongozi hao wakiendelea kuwa makauleni katika suala zima la kuzidisha kila uchao matumizi katika ulinzi na majeshi.

Picha za baadhi ya wajumbe wa bunge la Afrika Novemba 28, 2019. Picha/ Ken Walibora

Wajumbe wengine kwenye kongomano walisema kwamba miongoni mwa vikwazo vikubwa kwa mchakato wa kuleta amani barani Afrika ni makundi ya kigaidi, umaskini, ukosefu wa usawa na ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.

Walisisitiza kwamba vijana hutumiwa vibaya na viongozi kuendeleza vita vya ndani mwa nchi au na nchi nyingine kwa vile hawana ajira wala msingi mwema wa kiuchumi.

Kwa hiyo wabunge hao walipendekeza kupanga na kutekelezwa kwa mikakati kabamba kuwahamasisha vijana na kuwaundia nafasi za ajira. Aidha waliwashutumu wanaume kuwa ndio wanaoanzisha vita na kuviendeleza huku vijana wakipiganishwa na watoto na wanawake wakiathiriwa vibaya zaidi kwa kubakwa, kujeruhiwa na kuuawa.

Mwakilishi wa Jamhuri isiyotambuliwa ya Saharawi, Bi Suilman Hay Emhamed Elkaid alisema vita haviwezi kuisha katika eneo la Kaskazini Magharibi ya Afrika bila kutambuliwa rasmi kwa uhuru wa watu wa Saharawi.