Kamala Harris achangiwa $200 milioni za kampeni
WASHINGTON DC, AMERIKA
NAIBU wa rais nchini Amerika na mgombeaji wa kiti cha urais Kamala Harris, amechangiwa $200m (Sh26 bilioni) za kufanya kampeni.
Hayo yanajiri kufuatia Rais wa Amerika Joe Biden kutangaza kusitisha azma yake ya kutetea kiti chake dhidi ya mpinzani wake anayepeperusha bendera kwa tiketi ya Republican na ambaye kadhalika alikuwa rais wa zamani, Donald Trump.
Biden alimpisha Kamala kuwa mpeperushaji bendera akiwania urais katika chama cha Democratic.
Kamati ya kuongoza kampeni ya Kamala ilitangaza jumla ya pesa zilizokusanywa za kampeni kufikia Jumapili.
Aidha, kamati hiyo iliongeza kwamba kati ya pesa hizo zilizokusanywa, asilimia 66 ya waliochanga ni wahisani waliojitolea kuchanga peza za kampeni kwa mara ya kwanza katika mchakato wa uchaguzi wa mwaka 2024.
Isitoshe, zaidi ya wahisani 170,000 wamejitolea bila malipo kumsaidia Kamala katika shughuli za kumpigia debe.
“Kasi aliyo nayo pamoja na nguvu ni ishara tosha kwamba Kamala amejituma kuwania urais. Ni kinyang’anyiro kitakachokuwa kikiamuliwa na idadi ndogo ya kura kutoka katika maeneo machache tu,” akasema mkurugenzi wa mawasiliano kitengo cha kampeni, Michael Tyler.
Kwa upande mwingine, kitengo cha mawasiliano cha mwaniaji wa urais Donald Trump kiliambia wanahabari kwamba mapema mwezi Julai mwaka huu, kilikuwa kimechanga $331 milioni katika kipindi cha miezi mitatu, na kupiku $264 milioni, pesa ambazo zilikuwa zimechangishwa katika kampeni ya Rais Biden na wanachama wa mrengo wake wa chama cha Democratic katika muda sawa wa miezi mitatu.
Kamati ya kampeni ya Trump ilikuwa imekusanya $284.9 milioni pesa tasilimu kufikia mwisho wa Juni mwaka huu huku, nao mrengo wa Democratic ukikusanya pesa taslimu $240 milioni wakati huo.
Aliyekuwa spika katika bunge la Amerika, Nancy Pelosi, Kiongozi wa walio wengi katika bunge la Seneti, Chuck Schumer, Kiongozi wa wengi, Hakeem Jeffries, kiongozi wa walio wachache Jim Clyburn, aliyekuwa rais wa Amerika Bill Clinton na aliyekuwa katibu katika ikulu ya rais Hillary Clinton ni miongoni mwa viongozi waliotangaza kumuunga mkono Kamala.