Kimataifa

Museveni sasa adai Bobi Wine alipanga kuiba kura

Na REUTERS January 31st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

HUKU akionekana kukerwa na utata unaozingira ushindi wake, Rais Yoweri Museveni amedai kuwa mpinzani wake Robert Kyangulanyi maarufu kama Bobi Wine alichapisha kura milioni moja feki na nyingine milioni 1.7 kutoka Dubai ili kupata ushindi kwenye uchaguzi mkuu wa Januari 17.
Museveni, 81 alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo kwa asilimia 71.6 za kura huku Kyangulanyi akipata kura milioni 2.7.
Kiongozi huyo amesema kutumika kwa mfumo wa kielektroniki kwenye uchaguzi huo ndiko kulizuia njama ya upinzani kutumia njia ya udanganyifu katika kura hiyo.
Alidai kuwa kwa sasa hakuna upinzani Uganda kwa sababu wapigakura wameonyesha imani yao kwa kumpa kura kupitia NRM.
“Fahamu hakuna upinzani Uganda, hao wanaosema kunao wanajidanganya tu. Baada ya uchaguzi tuligundua walichapisha karatasi milioni moja za kupiga kura hapa barabara ya Nkuruma na milioni nyingine milioni 1.7 kutoka Dubai,” akasema Museveni.
 Kiongozi alisifu matumizi ya mitambo ya kielektroniki ya kupiga kura akisema ilimwokoa kushindwa kwa njia ya udanganyifu na Kyangulanyi.
 “Ndiyo mitambo hii ilikuwa na matatizo ya hapa na pale lakini kila mtu alipiga kura. Hivyo ndivyo nilifaulu kuwashinda wanangu Bobi Wine na Mafabi Nandala ambao wamekuwa wakijaribu kuwachanganya watu hapa,” akasema Museveni.
Aliwakashifu viongozi hao wa upinzani kwa kulenga familia yake na kumkashifu mwanawe Muhoozi Kainerugaba ambaye ni mkuu wa jeshi la Uganda kwa kuingilia uchaguzi huo.
Kyangulanyi bado hajulikani alipo lakini Muhoozi amesema kuwa wanamtaka akiwa hai au akiwa ameaga dunia.
 Museveni alikuwa akiwahutubia wanajeshi wakati wa kuchaguliwa kwa wawakilishi wao ambao watashirikiana na bunge jipya lililoingia mamlakani baada ya kura hiyo.
Mnamo Ijumaa, Muhoozi alichemsha mitandao kwa kudai kuwa ubalozi wa Uingereza Amerika ndio ulikuwa umemsaidia Kyangulanyi kuhepa kutoka nyumbani kwake Magere Wakiso mnamo Januari 16.
“Kwa raia wa Uganda tupo katika hali ambapo kiongozi wa upinzani amejiteka nyara na kutokana taarifa za kijasusi ambazo tumepata, amekuwa akisaidiwa na ubalozi wa Amerika. Tunasitisha ushirikiano wowote wa utawala wa sasa na ubalozi wa Amerika Kampala kwa sababu ubalozi wa nchi hiyo umekuwa ukitatiza uhusiano na Uganda tangu 2015,” akasema Muhoozi kwenye mitandao yake ya kijamii kabla ya kufuta chapisho hilo.
 Serikali iliagiza intaneti izimwe wakati wa uchaguzi kama sehemu ya kuzuia kusambazwa kwa jumbe za uchochezi na chuki.