Somalia yatoa msaada wa madaktari kuisaidia Italia kukabili corona
MASHIRIKA NA FAUSTINE NGILA
SERIKALI ya taifa la Somalia Jumatatu imethibitisha kwamba imetuma madaktari 20 nchini Italia kusaidia kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya corona ambavyo vimeua zaidi ya raia 10,700 nchini humo.
Msemaji wa serikali ya Somalia Bw Ismail Mukhtar Omar amesema madaktari hao kutoka Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Somali wamejitolea kuisaidia Italia bila malipo. Amesema awali wametoa misaada ya hudumza za udaktari katika baadi ya mataifa ya Ulaya.
“Madaktari hao 20 tayari wamesajiliwa nchini Italia na wanataajiwa kushirikiana na madaktari wengine kutoka mataifa mbalimbali kuisaidia Italia kuzima virusi vya corona,” alisema Bw Omar.
Ameeleza kuwa madaktari hao wametumwa humo kama mpango wa kidharura kufutia ombi kutoka kwa serikali ya Italia inayohitaji msaada ya kimataifa.
Somalia, ambayo kufikia Jumatatu ilikuwa na visa 3 vya corona, imepiga marufuku safari zote za ndege, kimataifa na za nchini humo, kama mojawapo ya mikakati ya kupunguza watu wanaoambukizwa maradhi hayo.