Kimataifa

Trump kuingia ikuluni itakuwa ni zao la propaganda mbaya

Na DOUGLAS MUTUA July 20th, 2024 2 min read

PROPAGANDA – ule uwezo wa kukoroga akili za watu zikadhani weupe ni weusi na weusi ni weupe – ni sanaa chafu mno.

Nasisitiza ni sanaa chafu kwa sababu inaweza kukusababisha uanze kujiuliza iwapo una akili timamu au la.

Kwa muda sasa, nimekuwa nikijiuliza maswali kuhusu uzee, ambao tumekuwa tukiambiwa si ugonjwa, nikajiuliza wazee ni wageni wa nani duniani.

Nimezama kwenye bahari ya luja kuhusu uzee baada ya kutanabahi kuwa labda mimi pia ni mwathiriwa wa propaganda inayoenezwa Amerika.

Uzee umetokea kupata kichapo kikali katika taifa hilo tajiri na lenye ushawishi zaidi duniani, kisa na maana umri wa Rais Joe Biden.

Mjomba Joe, kama anavyoitwa na wengi wanaompenda, ana umri wa miaka 82 na amegeuka king’ang’anizi wa kukatalia kwenye Ikulu ya White House.

Si kwamba hawezi kukaa humo kisheria akitaka, ila maoni ya wengi ni kwamba amekonga sana, hivyo anashinikizwa kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha urais kitakachofanyika Disemba.

Ninapokuandikia makala hii, dalili zote zinaonyesha kwamba huenda akajiondoa, hasa kwa kuwa wanaomshinikiza ni viongozi wa chama cha Democrat anachoongoza.

Bado haijajulikana iwapo Mkenya Mmarekani kwa jina Barack Obama, aliyekuwa rais wa Amerika huku Mjomba Joe akiwa makamu wake miaka kadha iliyopita, amemshinikiza Joe moja kwa moja ajiondoe.

Hata hivyo, wanaomshinikiza Mjomba Joe ni marafiki wa karibu wa Rais Obama, ambao walitumika katika serikali yake alipoongoza Amerika kwa haiba kubwa.

Je, hivi Rais Biden anashinikizwa kujiondoa kwa sababu ya uzee, kwani anakabiliana na nani? Mbeba mwenge wa chama cha Republican ni aliyekuwa rais, Donald Trump, ambaye alishindwa na Rais Biden miaka minne iliyopita.

Trump mwenyewe ana umri wa miaka mingapi? Ana 79, anaelekea kugonga 80. Kwa ufupi, kwa sababu Trump ameachwa na Rais Biden kwa miaka mitatu pekee, tunaweza kusema wote wawili ni wazee wa rika moja.

Jiulize kwa nini uzee wa Rais Biden unachukuliwa kama donda ndugu linalonuka vibaya, huku wa Trump, pamoja na dalili zote za kutookenaka kuwa na akili timamu, ukifumbiwa jicho.

Tatizo ni propaganda! Rais Biden, japo ana dalili za kusahausahau kwa sababu ya ukongwe, ameiongoza Amerika kwa ustaarabu wa kupigiwa mfano akilinganishwa na Trump alivyovuruga mambo.

Uchumi wa Amerika umekua vizuri tu wakati wa utawala wa Rais Biden, taifa hilo limeanza kuheshimika tena duniani, sikwambii alisimamia kwa weledi mkuu mpito wa kuondokana na janga la Corona.

Hayo yote yalikuwa yamemlemea Trump alipokuwa mwenyeji wa ikulu, lakini kwa sababu ana uwezo wa kukoroga akili za watu na kuwasahaulisha madhaifu yake, sasa umaarufu wake ni wa kaimati moto.

Kisa cha Biden na Trump kinanikumbusha athari za propaganda nchini Kenya tangu nilipokuwa mdogo. Enzi hizo tukiambiwa kuwa marehemu Daniel Moi alikuwa na saratani ya koo, eti angefia madarakani. Mzee wa Kanu huyo aliiongoza nchi kwa miaka 24, akastaafu na kuishi duniani kwa miaka 20 zaidi!

Wakati wa uchaguzi uliopita, tuliambiwa kuwa kinara wa Orange Democratic Movement (ODM) Bw Raila Odinga, ni mzee asiyeweza kuongoza nchi kutokana na ukongwe.

Waliomponda siku hizo sasa wanampigia debe ili apewe fursa ya kuongoza Afrika nzima!

Upo uwezekano mkubwa mno kwamba propaganda itawapa Wamarekani kiongozi asiyefaa. Hilo la kutofaa sina shaka nalo.

Hata hivyo, itakuwa bora iwapo dunia nzima itautumia utawala ujao wa Trump kama mfano mbaya wa mazao ya propaganda.

[email protected]