Kimataifa

Zuma apinga matokeo, ataka kura zirudiwe licha ya kuwa rais anaapishwa leo Jumatano

Na Na MASHIRIKA June 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

JOHANNESBURG, A. Kusini

ALIYEKUWA Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma sasa ameikosoa serikali mpya ya muungano iliyoundwa na Rais Cyril Ramaphosa na kuitisha uchaguzi mwingine.

“Sharti uchaguzi urudiwe. Uchaguzi mwingine ufanywe,” Zuma ambaye pia ni kiongozi wa chama kipya cha uMkhonto weSizwe (MK) alitoa pendekezo hilo Jumatatu.

Chama cha MK kiliibuka nambari tatu katika uchaguzi mkuu uliofanyika Mei 29 mwaka huu. Kimeapa kwamba wabunge wake wapatao 58 hawataunga mkono serikali mpya ya muungano.

Aidha, Zuma amewahi kusema kuwa chama chake hakitafanya mazungumzo na kile cha Afrika National Congress (ANC) endapo Rais Ramaphosa ataendelea kuwa kiongozi wake.

Ramaphosa alichaguliwa tena na wabunge Ijumaa iliyopita na kupata nafasi ya kuhudumu kwa muhula wa pili.

Hii ni baada ya ANC kuelewana kubuni muungano na chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) na vyama vingine vidogo.

“Idadi kubwa ya vyama vya kisiasa vinalalamika kuwa havikutendewa haki. Tunataka suala hili liangaliwe,” Zuma akasema.

Mahakama ya nje ya nchi

Rais huyo wa zamani aliwaambia wafuasi chama chake, MK, kwamba vyama vinavyolalamika vitawasilisha malalamishi yao katika mahakama ya nje ya taifa hilo.

Zuma alisema mahakama za Afrika Kusini haziaminiki kwani zinapendelea mrengo wa serikali.

“Tunaelekea katika mahakama ya kimataifa……. Ili majaji wa Afrika Kusini wasipate nafasi ya kusikiza kesi yetu,” akasema.

Rais huyo wa zamani alidai kuwa visa vingi vya udanganyifu vilifanyika katika vituo vya kupigia kura wakati wa uchaguzi mkuu wa Mei 29.

“Kwa hivyo, tunataka uchaguzi urudiwe ili tuone kura vizuri. Tunafahamu mengi kuhusu maovu yaliyotendeka katika uchaguzi uliopita. Baadhi ya kura ziliteketezwa,” Zuma akasema.