Habari

Kizaazaa kortini DNA kuonyesha mama ndiye mzazi halisi wa mtoto 'aliyeiba'

April 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na TITUS OMINDE

KULIKUWA na sarakasi katika mahakama ya Eldoret Jumatatu pale mahakama ilipoamuru kuwa mama ambaye alishtakiwa kuiba mtoto ndiye mama halisi wa mtoto husika.

Uamuzi huo wa mahakama ulitokana na matokeo ya uchunguzi wa DNA ambayo yaliwasilishwa mahakamani humo.

Ursillah Jeptoo alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya wizi wa mtoto kutoka kwa Lucy Chepkoech ambaye alidai kuwa mama wa mtoto huyo.

Chepkoech alikuwa ameambia mahakama kuwa yeye ndiye mama wa mtoto huyo wa miaka matatu.

Kupitia kwa wakili wake Chepkoech alidai kuwa mtoto huyo aliibwa kutoka kwake katika hospitali ya rufaa ya Kapsabet mnamo Aprili 24 mwaka wa 2015.

Ajabu ni kwamba Jeptoo amekuwa akishi na mtoto huyo tangu ajifungue yapata miaka mitatu zilizopita.

Jeptoo kupitia kwa wakili wake Ledisha Kipseei aliambia mahakama kuwa alijifungua mtoto huyo siku ambayo mlalamishi alidai kujifungua.

Mshtakiwa alionyesha mahakama stakabadhi za hospitali ya Racecourse mjini Eldoret ambako alijifungulia mtoto huyo walakini mlalamishi hakuwa na stakabadhi zozote kuonyesha alikojifungulia mtoto huyo.

Jeptoo alitiwa mbaroni mnamo Januari 25 kwa madai ya kuiba mtoto wa Chepkoech.

Mlalamishi alidai kuwa mtoto wake aliibwa kutoka hospitalini punde baada ya kujifungua lakini hakuonyesha stakabadhi za kuripoti kupotea kwa mtoto wake.

Mshtakiwa alikana mashtaka dhidi yake huku akitilia mkazo kwamba alijifungua mtoto huyo mnamo Aprili 24, 2015 katika hospitali ya Race Course mjini Eldoret ambapo amekuwa akimnyonyesha na kumlea tangu ajifungue.

Jeptoo aliwasilsiha vyeti vya kuzaliwa na stkabadhi nyingine muhimu mahakamani.

Mshtakiwa alitiwa mbaroni na polisi mnamo Januari 25 kwa madai ya kuiba mtoto. Kutoka kwa mwanamke mwingine.

Wakati pande zote mbili zilipofika mbele ya hakimu mkuu wa Eldoret Charles Obulutsa zilikubali kutoa chembechembe za damu ili kufanikisha uchunguzi wa DNA.

Akitoa uamuzi wake hakimu Obulutsa aliamuru mtoto kuwa mtoto huyo ni wake Jepto baada ya matokeo ya DNA kubainisha kwa aslimia 99 Jeptoo ndiye alikuwa mama wa mtoto huyo.

Mapema Januari mwaka huu mahakama iliamuru  Jeptoo kupewa haki ya kukaa na mtoto huyo wakati kesi ilipokuwa ikiendelea mahakamani kwani mlalamishi hakuwahifika kortini ila alikuwa akiwakilishwa na wakili wake.

Awali mlalamishi alikuwa amepinga matoeo ya DNA kwa madai kuwa hayakufanywa kwa njia ya uwazi.