HabariHabari za Kitaifa

Matatizo kila kona shule zikifunguliwa Jumatatu

Na CHARLES WASONGA, WINNIE ATIENO August 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

UTATA umegubika sekta ya elimu nchini kiasi kwamba, licha ya serikali kutuma pesa shuleni, huenda masomo yasianze Jumatatu baada ya walimu kuapa kuanza mgomo wao wa kitaifa.

Waziri wa Elimu Julius Migos alisema serikali imetoa jumla ya Sh21.8 bilioni kwa shule za msingi na upili kote nchini za kufadhili masomo katika muhula wa tatu, taasisi hizo zinapofunguliwa kwa muhula wa tatu.

“Pesa hizo zimegawanywa kwa njia ifuatayo katika ngazi tatu za elimu ya msingi, Sh1.62 bilioni ni za Elimu bila Malipo katika Shule za Msingi, Sh6.1 bilioni za Mpango wa Elimu Bila Malipo katika Shule za Upili za Msingi (JSS) na Sh14.1 bilioni za Mpango wa Elimu Bila Malipo katika Shule za Upili za Kutwa,” akasema waziri huyo kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Lakini vyama vya kutetea walimu katika shule za msingi na upili vimewataka wanachama wao kuanza kutofika shuleni muhula muhimu wa mitihani unapoanza.

Viongozi wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) na wenzao wa chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (Kuppet) wameshikilia watagoma hadi matakwa yao yote – kuhusiana na utekelezaji wa awamu ya pili ya makubaliano ya pamoja kuhusu nyongeza ya mishahara ya uboreshaji wa mazingira ya kazi (CBA) ya 2021 hadi 2025 – yatakapotekelezwa.

Miongoni mwa matakwa hayo ni; kupandishwa vyeo kwa walimu 130,000, kuajiriwa kwa walimu 20,000 zaidi na kuajiriwa kwa walimu 46,000 vibarua wanaofunza katika Shule za Upili za Msingi (JSS).

Mkutano kati ya Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Huduma za Walimu (TSC) Nancy Macharia na viongozi wa Knut na Kuppet, uliotishwa Jumanne kufikia makubaliano kuhusu suala hilo haukuzaa matunda yoyote.

Viongozi wa vyama hivyo, wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Knut Collin Oyuu na mwenzake wa Kuppet Akello Misori walisema, TSC haikuonyesha nia ya kutekeleza matakwa yao.

“Kwa sababu hatujafikia makubaliano, hatuna jingine ila kuwaambia wanachama wetu kwamba, mgomo utaendelea Jumatatu Agosti 26, 2024 ulivyopangwa,” akasema Bw Oyuu. Mnamo Ijumaa Agosti 16, wanachama wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la Kuppet lilifanya kikao na kuamua kwamba, mgomo utaendelea.

“Mkutano huo uliamua kuwa mgomo utaendelea ulivyopangwa na chama hiki kitaendelea kuwahimiza wanachama wake kuhakikisha mgomo huo unafaulu kwani walimu wanafaa kupewa haki yao,” akasema Bw Misori.

Wiki iliyopita, Rais William Ruto alitoa wito kwa mawaziri wa Elimu, Leba na Fedha pamoja na wakuu wa TSC kuketi na viongozi wa vyama vya elimu ili kupata suluhu kwa suala hilo.

“Ninataka mawaziri hawa watatu na TSC kufanya mkutano na viongozi wa Knut na Kuppet kwa lengo la kuzuia mgomo huu ambao bila shaka utaathiri masomo ya watoto wetu. Naamini kuwa wanaweza kukubaliana,” Dkt Ruto alisema katika Ikulu Ndogo ya Eldoret alipotumbuizwa na wanafunzi waliofanya vizuri katika Tamasha ya Kitaifa ya Muziki baina ya Shule.

Japo Waziri wa Leba Alfred Mutua aliwahi kufanya mkutano na viongozi wa Knut na Kuppet, mwenzake wa Elimu Bw Migos hajawahi kukutana na viongozi wa vya vyama hivyo.

Kwa upande wake, Bw Mbadi Alhamisi usiku alisema serikali haina pesa za kufadhili matakwa ya walimu.

Kwenye mahojiano katika runinga ya Citizen, waziri huyo aliongeza kuwa, serikali inakabiliwa na uhaba wa fedha kiasi kwamba, haiwezi kuwapa walimu 46,000 wa JSS ajira ya kudumu na kuwaajiri walimu wengine 20,000 wapya.

“Mwaka huu, hali imekuwa ngumu zaidi kwani serikali haina pesa za kuwaajiri walimu wapya, kuwapandisha vyeo na hata kuwapa ajira ya kudumu kwa walimu wa JSS,” Bw Mbadi akaeleza.

Wakati huo huo, wazazi wamepinga agizo la Wizara ya Elimu la kuwataka kuwasajili watoto kwa Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF).

Baadhi yao wamepuuza agizo hilo wakilitaja kama mzaha wakishikilia kuwa, sheria ya kubuni hazina hiyo imeharamishwa na mahakama na wabunge kuagizwa kuishughulikia upya.

Mnamo Ijumaa, Katibu wa Wizara ya Elimu Belio Kipsang’ aliagiza kuwa wanafunzi wote katika shule za msingi na upili wasajiliwe kwa SHIF kabla ya shule kufunguliwa Jumatatu.

“Usajili wa Wakenya kwa Hazina ya Afya ya Kijamii ulianza Julai 1, 2024 kama njia ya kuwezesha kufikiwa kwa Mpango wa Afya kwa Wote.

Kwa hivyo, wanafunzi wote wanahitajika kusajiliwa kama wategemeaji wa wazazi wao kabla ya tarehe ya shule kufunguliwa kwa muhula wa tatu wa mwaka wa masomo wa 2024,” Dkt Kipsang’ akasema.

Katibu huyo alisema usajili huo unaweza kufanywa kwenye majukwaa ya mitandaoni kupitia tovuti ya www.sha.go.ke au www.afyangua.go.ke au kwa njia ya simu kupitia nambari *147#.