Habari

Mbunge alia kukosa ndege ya Addis Ababa kushuhudia kura za AUC

Na CECIL ODONGO February 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE wa Muhoroni James Onyango Koyoo Alhamisi alilalamika kuwa ndege zote zinazoelekea Addis Ababa Ethiopia zimejaa, hali ambayo imemkosesha nafasi ya kuhudhuria uchaguzi wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Bw Koyoo pia aliwaonya wale ambao wanaeneza habari mitandaoni kuwa zaidi ya wabunge 100 waliosafiri Ethiopia walitumia pesa za umma, akishikilia kuwa walitumia hela zao kibinafsi na suala hilo halifai kuzua mjadala.

“Mimi sina furaha kwa sababu nimejaribu kadri ya uwezo wangu na mali yangu kuenda Addis Ababa lakini ndege ndiyo nimekosa. Lau ningekuwa nimekodisha mapema, ningekuwa huko. Sasa ndege zimejaa na sijapata kabisa,” akasema Bw Koyoo ambaye ni mbunge wa ODM anayehudumu muhula wa tatu.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo alisema kuwa ana imani kuwa Bw Odinga atawashinda wapinzani wake wawili kwenye uchaguzi wa uenyekiti wa AUC mnamo Jumamosi. Alikuwa akizungumza eneobunge la Langáta baada ya kutembelea familia ya marehemu mtangazaji nguli Leonard Mambo Mbotela.

“Hata kama najuta kwa kukosa ndege, jambo moja ambalo nawahakikishia ni kuwa Baba (Raila) atashinda kura ya AUC na kutakuwa na sherehe kubwa hapa Kenya,” akaongeza mbunge huyo.

Aliwaendea baadhi ya Wakenya ambao wamekuwa wakimwombea Bw Odinga dua mbaya mitandaoni akiwataja kama wale ambao si wazalendo.

“Hili suala la gharama linawaghadhabisha Wakenya bure kwa sababu waliolipiwa pesa na serikali ni Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah na mbunge wa Nyando Jared Okello ambao watakuwa wakisimamia uhesabu wa kura upande wa Raila,

“Rais William Ruto, Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Katibu wa wazira ya masuala ya kigeni Korir Singóei pia wamelipiwa gharama na serikali. Wabunge na wengine ambao wapo kwenye ziara hiyo wote wamelipiwa pesa na serikali,” akasema Bw Koyoo.