Miaka 10 ya kafyu: Wakazi sasa walilia safari za usiku
WASAFIRI wanaotumia barabara kuu ya Lamu-Witu-Garsen katika Kaunti ya Lamu wanalalamikia kuendelezwa kwa marufuku ya safari za usiku eneo hilo, ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka 10 sasa.
Mnamo Julai 2014 serikali kuu kupitia idara ya usalama ilipiga marufuku safari zote za usiku kwa magari ya uchukuzi wa umma (PSV) na pia yale ya kibinafsi.
Hatua hiyo ilitokana na kukithiri kwa mashambulio na mauaji yaliyokuwa yakitekelezwa na Al-Shabaab kwa wasafiri na walinda usalama barabarani.
Katika mahojiano na Taifa Leo, watumiaji wa barabara hiyo, ikiwemo madereva, wasafiri wa magari na wale wa miguu na pikipiki, walitaja kuendelezwa kwa marufuku ya usiku barabarani kuwa jambo linaloathiri pakubwa shughuli zao za kila siku za uchukuzi.
Uchunguzi wa Taifa Leo ulibaini kuwa baadhi ya mabasi na matatu zinazotoka majira ya saa tano za usiku mjini Mombasa kuelekea Lamu hulazimika kusimama eneo la Minjila hadi kupambazuke ndipo waruhusiwe kuendelea na safari zao.
Bw Swaleh Said, mmoja wa makondakta wanaohudumu kwenye barabara ya Lamu-Witu-Garsen, aliomba kuwepo na mpangilio utakaohakikisha safari za usiku barabarabani ni zenye kufululiza bila kutatizwa.
“Twaipongeza serikali kwa juhudi zake za kuimarisha usalama barabarani. Ila hii marufuku ya muda mrefu ya safari za usiku imetuchokesha. Iondolewe. Twataka kuona usafiri wa usiku ukiendelezwa kikamilifu barabarani,” akasema BW Swaleh.
Ahmed Abdalla, msafiri, alisema kuendelea kuwepo kwa marufuku ya usiku barabarani ni kuhatarisha maisha yao, hasa wakati kunapotokea dharura kama vile mgonjwa anayehitaji kusafirishwa haraka nje ya Lamu kwa matibabu.
“Twahangaika si haba punde watu wetu wanapogonjeka na kupewa rufaa nje ya Lamu usiku. Hilo linamaanisha mgonjwa ambaye huenda yu mahututi asubiri hadi kuche ndipo asafirishwe. Safari za usiku zirejelewe ili kupunguza presha hizo,” akasema Bw Abdalla.
Kudumisha usalama
Omar Shekuwe, ambaye ni mshikadau katika sekta ya utalii, alisema kuondolewa kwa marufuku ya usiku kwenye barabara ya Lamu-Witu-Garsen kutasaidia kusafiri kiurahisi kwa watalii hasa msimu huu ambao ni kipindi cha watalii wengi wanaozuru Lamu na Kenya kwa jumla.
Akijibu lalama hizo, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Wesley Koech alishikilia kuwa dhamira ya marufuku hiyo ya usiku ni kuhakikisha wanaotumia barabara ya Lamu-Witu-Garsen wanalindwa vilivyo.
Bw Koech hata hivyo aliahidi kuweka mkutano utakaokutanisha maafisa wa idara ya usalama na ile ya uchukuzi hivi karibuni ili kujadiliana ni jinsi gani marufuku hiyo itaondolewa.
“Nafahamu kuwa marufuku imekuwepo baada ya visa vya magaidi kushambulia wasafiri barabarani kushuhudiwa eneo hili. Mwezi au miezi miwili ijayo tutakutana, kujadiliana na kutathmini hali ilivyo ya usalama barabarani. Tutajua hapoendapo itakuwa ni salama kuondoa marufuku ya usiku,” akasema Bw Koech.