Mlima Kenya utahama Jubilee – Moses Kuria
Na NDUNGU GACHANE
MIVUTANO katika Chama cha Jubilee umezidi kutokota huku Mbunge wa Gatundu Kusini akitangaza mipango ya kuunda chama kipya kitakachotetea maslahi ya jamii za Mlima Kenya.
Bw Kuria Jumapili alieleza wazi kwamba uamuzi uliochangia kuvunjwa kwa chama cha zamani cha The National Alliance (TNA) ambacho Rais Uhuru Kenyatta alitumia kuwania urais mwaka wa 2013, uliacha Mlima Kenya bila namna ya kujitetea vilivyo kisiasa.
TNA kilivunjwa pamoja na vyama vingine vya muungano uliokuwepo wa Jubilee, kikiwemo Chama cha United Republican Party (URP) kilichoongozwa na Naibu Rais William Ruto, kuunda Chama cha Jubilee ambacho kilishinda urais mwaka wa 2017.
Kauli ya Bw Kuria imetokea wakati ambapo joto la kisiasa linachacha katika Chama cha Jubilee kati ya mrengo unaounga mkono azimio la Dkt Ruto kuwania urais 2022, almaarufu ‘Team Tangatanga’, na kundi jingine linalokashifu kampeni za mapema almaarufu kama ‘Team Kieleweke’.
Wandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakidai kwamba kuna njama zinazoendelezwa kumzuia Dkt Ruto kufanikiwa katika uchaguzi wa urais ifikapo mwaka wa 2022 ikiwa ni pamoja na kuvuruga Jubilee.
“Tulikosea wakati tulipovunja chama chetu cha The National Alliance kwa sababu Jubilee ni chama kisicho na mwelekeo ambacho hatuwezi kutumia kufanya mipango yetu ya Mlima Kenya. Nitasajili chama kipya cha kisiasa ambacho kitawapa viongozi wa Mlima Kenya nafasi ya kufanya mipango kuhusu masilahi yetu ya siku za usoni serikalini,” akasema Bw Kuria.
Alikuwa akizungumza katika Kanisa Katoliki la Sabasaba, Kaunti ya Murang’a ambapo aliandamana na viongozi wengine wa Jubilee akiwemo Mbunge wa Kandara, Bi Alice Wahome na mwenzake wa Maragua, Bi Mary Waithira pamoja na Seneta wa Murang’a, Bw Irungu Kang’ata.
Bw Kang’ata alikiri kwamba siasa zinazoendelezwa zimesababisha mgawanyiko wa viongozi na sasa chama kinaelekea mahali pabaya.
“Chama chetu kinaelekea pabaya kwa sababu pande mbili za Tangatanga na Kieleweke zinasababisha chuki miongoni mwa wale wanaochukuliwa kuwa wapinzani wao,” akasema.
Suala la iwapo Dkt Ruto atatumia Chama cha Jubilee kuwania urais 2022 limekuwa kwenye ndimi za baadhi ya wafuasi wake na wachanganuzi wa siasa kwa muda mrefu hasa tangu misukosuko ilipozidi katika Jubilee kuutokana na muafaka wa Rais Kenyatta na Kiongozi wa Upinzani, Bw Raila Odinga.
Wakati mmoja, ilifichuka kwamba viongozi wanaoegemea upande wa Naibu Rais walisajili vyama vipya na kushukiwa kuwa hayo yalikuwa maandalizi ya kujitafutia makao salama endapo Dkt Ruto ‘atasalitiwa’ na viongozi wa Jubilee wanaotoka Mlima Kenya.
Bi Wahome alitoa wito kwa Rais Kenyatta kuingilia kati ili kutuliza hali chamani na kuepusha mashua ya Jubilee kuzama katika dhoruba kali inayoshuhudiwa.
“Tulipiga kura kwa wingi kuwachagua Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto na tunamtegemea kiongozi wa chama kudhibiti hali iliyopo chamani kwa sasa,” akasema.
Ripoti zaidi na Valentine Obara