Mmoja ajeruhiwa wafuasi wa mbunge, mpinzani wakipigana Homa Bay
MTU mmoja anaendelea kuuguza majeraha katika hospitali moja ya kibinafsi mjini Oyugis baada ya makundi mawili ya vijana Jumatatu kupigana kwenye hafla ya mazishi Kaunti ya Homa Bay.
Baadhi ya magari pia yalivunjwa vioo wakati wa tukio hilo kwenye kijiji cha Kobour, Wadi ya Kamagak Magharibi. Inadaiwa makundi hayo mawili ya vijana yalipigana kutokana na tofauti za kisiasa.
Polisi jana walisema wameanzisha uchunguzi kuhusu kile ambacho kilisababisha ghasia hizo huku wakiapa kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya yeyote ambaye atapatikana na hatia.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Rachuonyo Kusini Philemo Saera, vijana ambao walipigana walikuwa wafuasi wa Mbunge wa Kasipul Ong’ondo Were na mpinzani wake Philip Aroko.
Bw Aroko ametangaza nia ya kumbandua Bw Were ambaye amehudumu kama mbunge wa Kasipul tangu 2017 katika kura ya 2027.
Wanasiasa hao wawili walikuwa kwenye mazishi hiyo wakati vurugu hizo.
“Wote walikuwa wamewasafirisha wahuni. Ni kati ya vijana ambao walikuwa wakipigana,” akasema Bw Saera.
Kwa mujibu wa kamanda huyo bado hajafahamu maelezo ya ndani kuhusu kilichotokea. Walioshuhudia tukio hilo hata hivyo walidai wafuasi wa mrengo mmoja walijaribu kutimua wenzao kutoka viti walivyovikalia na vita vikazuka.
Picha ambazo zilienea mitandaoni zilionyesha baadhi ya vijana wakiwa wamejihami kwa panga na silaha butu. Kwenye video ambayo pia ipo mitandaoni afisa mmoja wa utawala alionekana akiwabembeleza vijana hao wadumishe amani.
Katika video hiyo makundi hayo mawili yalikabiliana huku kijana mmoja akijeruhiwa na magari yakipasuliwa vioo. Bw Saera alisema kuwa mbunge huyo na mpinzani wake hata hivyo hawakujeruhiwa katika patashika hizo.
“Tunashughulikia suala hili na tutaamua hatua kali zaidi kuwahukumu wahusika,” akasema
Si mara ya kwanza ambapo vijana wanaoegemea wanasiasa mbalimbali wanakabiliana kwenye hafla za mazishi. Bw Saera alisema mtindo huo unaongezeka Homa Bay na akasema wanasiasa ndio wana kazi ya kuwadhibiti wafuasi wao.
“Viongozi wanastahili kuyaendeleza maeneo yao badala ya kuonyeshana ubabe kwa kuwatumia vijana kupigana na wapinzani,
“Watakuwa wakijeruhiwa kisha wajigharimie matibabu. Majeraha mengine yanaweza kuishia kuwaacha na ulemavu huku wanasiasa nao wakiendelea na maisha yao ya kawaida,” akasema.
Kwa mujibu wa Newton Ogada ambaye anatoka Kasipul, tabia ya wanasiasa kupigana kwenye mazishi inasikitisha na ni utovu wa heshima.
“Badala ya kuwafariji wanafamilia, wao wanatumia vijana kupigana na kuonyesha nani maarufu. Hii tabia lazima ikome,” akasema Bw Ogada.