HabariSiasa

Mudavadi avuna wanachama 350 kutoka Jubilee

August 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

CHAMA cha Musalia Mudavadi, ANC, Jumanne kimeendelea kuvuna wafuasi wa Rais Uhuru Kenyatta katika Kaunti ya Murang’a baada ya wanachama wengine 100 kumwendea kutoka Jubilee.

Katika siku mbili sasa mfululizo, chama hicho cha ANC kimejipa wafuasi 350 kutoka Jubilee.

Baada ya aliyekuwa mbunge wa Maragua Peter Kamande kugura Jubilee Jumatatu na kuingia kwa ANC akiwa na wafuasi 250, leo imekuwa ni zamu ya aliyekuwa diwani wa Gitugi Bw Duncan Njuguna kurukia basi la Mudavadi akiwa na wafuasi 100 katika hafla mjini Kenol.

Katika hali zote mbili, walipokelewa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Jubilee katika Kaunti hiyo Bw Simon Gikuru aliyejiunga na Mudavadi miezi kadha iliyopita.

Wote walisema kuwa chama cha Jubilee kwa sasa kimekumbwa na migogoro ya uongozi na pia kutokuwa na demokrasia ya kujieleza.

Aidha, walisema kuwa chama hicho kimegeuzwa kuwa miliki ya wachache ambao wakiamua kukutimua au kukuvua madaraka, haki yako ya kujieleza na kufuata mrengo utakao inahujumiwa kwa kiwango kikuu.

Wadadisi walisema kuwa uhame huo wa wafuasi wa Jubilee hadi kwa mrengo wa Mudavadi ni ishara tosha kuwa Mlima Kenya hautakuwa na ule msimamo mkali wa jadi wa kuunga tu mtu wa nyumbani mkono.

“Eneo hili sasa liwazi kuchumbiwa na aliye na maono mema kwetu. Raila Odinga akija na atuchumbie vitamu, tutafuata yeye. Dkt William Ruto akija na atuchumbie vilivyo…wengine wote katika kinyang’anyiro cha urais 2022, sisi tuko tayari bora tuahidiwe mahari tamu ya poza hiyo kisiasa,” akasema Mwenyekiti wa Gikuyu, Embu na Ameru (Gema) Lawi Imathiu.

Bw Kamande alisema kuwa kujiunga na ANC kwa sasa ni ishara tosha kuwa Mlima Kenya hautaachwa nyuma katika kuafikia lengo la kuungana na Wakenya wengine chini ya mwavuli wa BBI.

“Mugikuyu akiungana na Mulembe kwa sasa tutajivunia wingi wa mianya ya kibiashara na hata kura. Huu sasa sio wakati wa kuendeleza ule ujinga wa kikabila katika hali zetu za kimaisha kwa kuwa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 zilitupevusha macho kuwa sisi wote tuko na mwili na damu wa kudhulumika katika utengano,” akasema.

Mchanganuzi wa siasa za Mlima Kenya Prof Ngugi Njoroge aliambia Taifa Leo kuwa uamuzi wa wafuasi hao kuingia ANC wala sio chama kingine ni suala nyeti.

“Mudavadi hajakuwa na ule uhasama na watu wa Mlimani na haonekani akiwa wa ghasia. Ni mpole wa maongezi na hisia na hapigani na wanasiasa wengine hivyo basi kujiangazia kama anayeweza kuaminiwa na amani ya nchi. Pia, hujiangazia kama anayependa sana masuala ya utawala bora kiuchumi hivyo basi jamii za Mlima Kenya ambazo hujumuisha wafanyabiashara kwa kiwango kikuu wakimwona kama mfaafu,” akasema.

Alisema kuwa muungano wa Mulembe na Gema ukiundwa bila unafiki na kuwe na kujituma kuudumisha, basi wengine wajiandae tu kuwa upinzani kwa kuwa ushindi ni kura na kura ni watu akiongeza kuwa Magharibi na Mlima Kenya kuna zaidi ya asilimia 50 ya wapiga kura.