Ndoto ya Raila ilivyokosa kutimia urais ukimponyoka mara tano
KIFO cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, kilichotokea Jumatano, Oktoba 15, 2025 akiwa na umri wa miaka 80, kimefunga rasmi ukurasa wa safari yake ya muda mrefu ya kuwania urais, safari ambayo alijaribu mara tano bila mafanikio.
Bw Odinga, ambaye kwa muda mrefu aliitwa “fumbo la siasa za Kenya,” alijitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais katika miaka ya 1997, 2007, 2013, 2017 na 2022, lakini ndoto yake ya kuingia Jumba la Mlimani – Ikulu haikutimia.
Kwa takriban miongo minne, Raila alikuwa na ufuasi mkubwa kote nchini, na jina lake lilikuwa na ushawishi wa kipekee katika siasa za kila uchaguzi mkuu.
Kampeni nyingi nchini ziliundwa ama kwa kumuunga mkono (Raila-mania) au kwa kumpinga (Raila-phobia).
Wafuasi wake walivutiwa na misimamo yake ya mageuzi, na msimamo wake wa kuwatetea wanyonge, hasa kutoka jamii zilizohisi kunyanyaswa na tawala zilizopita ambazo mara nyingi zilihusisha makabila mawili makuu nchini.
Katika uchaguzi mkuu wa 2007, Raila aliingia ulingoni kama mgombea aliyeonekana kuungwa mkono sana, na alipoteza kwa tofauti ndogo dhidi ya Rais wa wakati huo, Mwai Kibaki, katika uchaguzi uliobishaniwa sana.
Matokeo ya uchaguzi huo yalisababisha ghasia mbaya zaidi za baada ya uchaguzi kuwahi kushuhudiwa nchini, ambapo zaidi ya watu 1,000 waliuawa na maelfu wakafurushwa makwao.
Wafuasi wake waliamini kuwa aliibiwa ushindi. Chama chake cha ODM kilipata viti vingi bungeni, kikimshinda Kibaki ambaye alikuwa akiwania kwa tiketi ya PNU.
Pia soma: https://taifaleo.nation.co.ke/habari/habari-za-kitaifa/raila-odinga-amefariki-dunia-akiwa-india/
Kupitia mazungumzo ya amani yaliyoongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, marehemu Kofi Annan, Raila aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya mseto iliyoanzishwa ili kurejesha utulivu.
Katika uchaguzi wa 2022, Raila tena alionekana kuwa miongoni mwa wagombeaji waliopigiwa upatu kushinda, safari hii akiungwa mkono na Rais aliyekuwa madarakani, Uhuru Kenyatta, ambaye alikuwa amemtema Naibu wake, William Ruto.
Kwa wafuasi wake, huo ulikuwa wakati mwafaka wa hatimaye kuingia Ikulu, hasa kutokana na uungwaji mkono wa serikali na ufuasi wake wa jadi. Lakini kwa mara nyingine tena, alishindwa na Dkt Ruto, ambaye alipata asilimia 50.49 ya kura dhidi ya asilimia 48.85 za Raila.
Bw Raila alipinga matokeo hayo katika Mahakama ya Juu zaidi nchini, lakini jopo la majaji saba liliidhinisha ushindi wa Dkt Ruto.
Baadaye, Waziri Mkuu huyo wa zamani alikubali kufanya kazi na Rais Ruto, na hatua hiyo ilisababisha kuundwa kwa serikali ya ushirikiano ambapo baadhi ya wafuasi wake walipewa nyadhifa serikalini.
Alizaliwa Januari 7, 1945, akiwa mwana wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Kenya, Jaramogi Oginga Odinga. Raila aliwahi kuwa Mbunge wa Lang’ata kuanzia mwaka 1992 hadi 2013.
Alishinda ubunge kwa mara ya kwanza kwa tiketi ya chama cha Ford-Kenya 1992, akakitetea tena kwa tiketi ya NDP mwaka 1997, Narc mwaka 2002, na ODM mwaka 2007.
Kazi yake ya kwanza serikalini ilianza mwaka 1974 alipoajiriwa kama Meneja wa Viwango katika Shirika la Viwango la Kenya (KeBS), na kupandishwa kuwa Naibu Mkurugenzi hadi alipokamatwa mwaka 1982 kwa sababu za kisiasa – chini ya utawala wa Rais Daniel Arap Moi wakati huo.
Aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani kwa miezi saba na baadaye kushtakiwa kwa uhaini, lakini badala yake alifungwa bila kesi kwa miaka sita. Akiwa kizuizini, mama yake alifariki dunia mwaka 1984.
Pia soma: https://taifaleo.nation.co.ke/habari/tanzia-maombolezo-ya-baba-raila-odinga/
Rais wa wakati huo Daniel arap Moi aliamuru aachiliwe Februari 6, 1988, lakini alikamatwa tena Septemba mwaka huo huo na kufungwa tena hadi Juni 12, 1989.
Aidha, alikamatwa tena Julai 5, 1990, pamoja na viongozi Kenneth Matiba na Charles Rubia wakati wa kampeni ya kutaka vyama vingi. Aliachiliwa Juni 21, 1991, kisha akakimbilia Norway kuzuia kukamatwa tena.
Alirejea Kenya Februari 1992 na kujiunga na Ford ambapo alichaguliwa kuwa Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Jumla ya chama.
Alishinda ubunge wa Lang’ata mwaka 1992. Baada ya kifo cha baba yake mwaka 1994, alijaribu kuwania uenyekiti wa Ford-Kenya dhidi ya Michael Wamalwa Kijana lakini akashindwa.
Alijiuzulu kutoka Ford-Kenya na kujiunga na NDP, na mwaka 1997 akawania urais na kumaliza wa tatu, huku akitetea kiti chake cha ubunge.
Kisha akaunganisha NDP na KANU ya Rais Moi, na baadaye alihudumu kama Waziri wa Kawi kati ya mwaka 2001 na 2002.
Aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa KANU kabla ya kutofautiana na Moi, ambaye alimchagua Uhuru Kenyatta kuwa mrithi wake mwaka 2002.
Alijitoa KANU na kujiunga na LDP, ambayo kisha iliungana na NAK ya Mwai Kibaki kuunda muungano wa NARC uliomshinda Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa 2002.