Obado ana kesi ya kujibu kuhusiana na mauaji ya Sharon, korti yasema
ALIYEKUWA Gavana wa Migori Okoth Obado na watu wengine wawili wamepatikana na kesi ya kujibu kuhusiana na mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno, mnamo Septemba 2018.
Jaji wa Mahakama Kuu Cecilia Githua, alimhusisha Bw Obado, aliyekuwa msaidizi wake Bw Michael Oyamo na Bw Caspal Obiero ambaye ni diwani wa zamani wa kaunti ya Migori na mauaji ya kinyama ya Bi Otieno ambaye mwili wake ulitupwa msituni.
“Baada ya kuchambua ushahidi na taarifa zilizotolewa na mawakili na stakabadhi zilizowasilishwa mbele yangu, nimeamua kuwa kuna ushahidi wa kutosha wa kushtakiwa kwa watatu hao kwa kosa la kwanza (mauaji ya Sharon),” akasema Jaji huyo.
Jaji Githua, hata hivyo, alisema hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuwashtaki watatu hao kwa mauaji ya mtoto wa Sharon ambaye hakuwa amezaliwa.
Mimba hiyo ilikuwa ya majuma 28 na mahakama ilisema kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka haukuhimili kesi ya mauaji dhidi ya watatu hao.
Kesi hiyo itatajwa mnamo Februari 25 wakati ambapo washtakiwa wataamua ikiwa watatoa ushahidi baada ya kuapishwa au la. Aidha, wataamua ikiwa watawaita mashahidi wowote wa kuwatetea.
Marehemu Sharon na mwanawe aliyekuwa tumboni waliuawa usiku wa Septemba 3, na Septemba 4, 2018 katika eneo la Owade, Karachuonyo, Kaunti ya Homa Bay.
Aliuawa baada ya kutekwa nyara pamoja na mwanahabari aliyefaulu kutoroka, baada ya kudaiwa kuruka kutoka kwa gari lililokuwa likiwasafirisha.
Bw Obado alishtakiwa kwa mauaji ya Sharon mnamo Septemba 24, 2018. Alizuiliwa kwa miezi kadhaa kwenye rumande ya polisi kabla ya kuachiliwa kwa dhamana kufuatia agizo la Mahakama ya Rufaa.
Watu 42 walitoa ushahidi katika kesi hiyo.
Bw Obado alijitetea akisema kuwa siku ambayo Sharon aliuawa alikuwa nyumbani kwa kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Mwanasiasa huyo alidai kuwa alikamatwa kutokana na presha kutoka kwa umma. Hii ni licha ya kwamba kukamatwa kwake kulimwathiri kama mtu binafsi, familia yake na wakazi wa kaunti ya Migori aliowaongoza kama gavana wao.