ODM mbioni kuimarisha umaarufu Magharibi
BARACK ODUOR na GAITANO PESSA
CHAMA cha ODM kiko mbioni kuhakikisha kimedumisha umaarufu wake eneo la Magharibi baada ya wanasiasa wakuu katika jamii ya Waluhya kuanzisha mchakato wa kuunda chama kimoja na kujiondoa katika muungano wa NASA.
Jumamosi, viongozi wakuu wa ODM waliwashutumu viongozi wa Ford-Kenya na ANC kwa kuunda miungano mipya kwa ajili ya siasa za 2022, badala ya kulenga maridhiano.
Katika eneo la Homa Bay, kiongozi wa wachache Bungeni John Mbadi aliwapuzilia mbali washirika wengine ndani ya NASA kwa kusema wanapinga maridhiano ya hivi majuzi kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
“Ni wao wanapinga maridhiano, lakini ningependa kuwaambia wanaharibu muda wao. Viongozi hao wawili wamezama ndani ya makubaliano hayo na hakutakuwa na mjadala, na sio kwa sababu ya 2022,” alisema Bw Mbadi.
Mbunge huyo alikuwa akimshambulia kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ambaye amebadilisha jina la chama hicho kuwa One Kenya Movement.
Alisema ni mapema mno kwa vyama vya kisiasa katika upinzani kuanza kuunda miungano na kusambaratisha miungano mingine kwa sababu ya uchaguzi wa 2022.
Alisema uchaguzi huo utashawishiwa na mambo mengi na sio salamu tu.
“Uchaguzi wa mwaka jana ulileta mgawanyiko mkubwa, kiongozi wetu Raila Odinga aliamua kuridhiana na kuunda mkataba na Rais Uhuru Kenyatta. Hivyo, wenzetu kuondoka sasa katika muungano kwa sababu ya siasa za 2022 hawaoni mbali,” alisema Bw Mbadi wakati wa sherehe za kutoa zawadi katika Shule ya Msingi ya Wasara, katika Kisiwa cha Rusinga.
Tangu Rais Kenyatta na Raila Odinga waliporidhiana mwezi jana, vyama vya ANC, Wiper na FORD –Kenya vimeelezea kutoridhika kwao kuhusiana na mkataba kati ya viongozi hao,wakisema wamekuwa gizani.
Licha ya kuwa muungano wa upinzani, NASA, kusalia, matamshi ya hivi majuzi ya baadhi ya washirika wake yanaashiria kuwa muungano huo unaelekea kusambaratika.
Kiongozi wa FORD-Kenya Moses Wetangula na mwenzake wa ANC Musalia Mudavadi wamedokeza mpango wa kuunganisha vyama vyao, kukifanya kimoja, baada ya kutofautiana na ODM, chama tanzu cha muungano wa NASA.
Viongozi hao wanataka kujitenga na ODM kwa kumshutumu kiongozi wake Raila Odinga kusaliti muungano wa NASA kwa kufanya mkataba na Rais Kenyatta.
“Kilicho muhimu sasa ni maridhiano miongoni mwa Wakenya, na sio kuunda vyama vya kisiasa ili kuingia mamlakani,” alisema Mbadi.
Katika eneo la Busia, Mwakilishi wa Kike Florence Mutua(ODM) alipuzilia mbali mpango wa kuungana kwa FORD-Kenya na Amani National Congress, kwa kusema muungano huo hauwezi kuwaunganisha Wakenya.