Habari

Ruto ajipigia debe na mradi wa NYOTA unaofadhiliwa na Benki ya Dunia

Na RUTH MBULA January 31st, 2026 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto, kwa sasa anazunguka maeneo mbalimbali nchini kugawa mamilioni kwa vijana kupitia mradi wa National Youth Towards Advancement (NYOTA) unaolenga kuwainua kiuchumi.
Mnamo Alhamisi, Rais Ruto alikuwa Kaunti ya Kisii ambako zaidi ya vijana wajasiriamali 8,000 kutoka kaunti za Kisii, Nyamira na Migori walinufaika na jumla ya Sh220.5 milioni kama mtaji wa kuanzisha biashara.
Rais alieleza kuwa katika awamu ya kwanza ya mradi huo, kila anayenufaika atapokea Sh25,000.
Kati ya kiasi hicho, Sh22,000 zitawekwa moja kwa moja kwenye akaunti ya Pochi la Biashara kwa matumizi ya biashara, huku Sh3,000 zikiwekwa katika akaunti ya akiba ya Haba na Haba inayosimamiwa na Hazina ya Kitaifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF).
Awamu ya pili itahusisha kutolewa kwa Sh25,000 nyingine kwa kila anayenufaika, na hivyo kufanya jumla ya msaada wa kuanzisha biashara kufikia Sh50,000 kwa kila kijana.
Hata hivyo, mpango huo umeibua maswali kutoka kwa wakosoaji wanaohoji chanzo cha fedha hizo na iwapo zilitengwa rasmi katika bajeti, hasa ikizingatiwa kuwa serikali imekuwa ikiwasilisha NYOTA kama mradi wake maalum.
Taarifa za kuaminika zinaonyesha kuwa mradi wa NYOTA unafadhiliwa na Benki ya Dunia, ambayo imejitolea kutoa dola milioni 229 za Amerika, na mpango huo unatarajiwa kuendelea hadi mwaka wa 2028.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa kwenye tovuti ya Projects.Worldbank.org, ufadhili huo ulitangazwa Januari 2023 na kuidhinishwa Juni mwaka huo kama upanuzi wa mpango wa awali wa Kenya Youth Employment and Opportunities Program (KYEOP).
Mradi huu sasa unatekelezwa katika kaunti zote 47.
NYOTA unawalenga vijana wasio na ajira na walio katika mazingira magumu wenye umri wa miaka 18 hadi 29, na hadi miaka 35 kwa vijana wanaoishi na ulemavu waliosajiliwa na Baraza la Kitaifa la Watu Wenye Ulemavu.
Benki ya Dunia inasema kuwa mpango huo unawalenga hasa vijana walio na kiwango cha elimu kisichozidi cha sekondari, na unatekelezwa kote nchini.
Ili kufuzu, walengwa lazima wawe raia wa Kenya, wasiwe wameendelea zaidi ya Kidato cha Nne, wawe na kitambulisho cha taifa pamoja na laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina lao.
Mradi huu unaweka mkazo kwa vijana ambao mara nyingi hutengwa katika mipango ya kiuchumi, wakiwemo wanaoishi maeneo ya mashinani, makundi yaliyotengwa, vijana wenye ulemavu, akina mama vijana, wakimbizi wa ndani, vijana wanaoishi na virusi vya Ukimwi, jamii za wachache na makundi mengine yaliyo katika mazingira magumu.
Usajili wa NYOTA unafanywa kwa kutumia simu ya mkononi kwa kubonyeza *254# na kufuata maagizo yanayotolewa.
Kulingana na taarifa zilizochapishwa kwenye tovuti ya mradi, NYOTA inalenga kuboresha uwezo wa vijana kupata ajira na kupanua fursa za kiuchumi.
Vijana wanaokumbana na changamoto za kutumia mfumo wa kidijitali wanaelekezwa kutafuta usaidizi katika afisi za Kaunti au Kaunti Ndogo za Idara ya Masuala ya Vijana na Uchumi Bunifu, au katika afisi za Mamlaka ya Biashara Ndogo na za Kati zilizo karibu nao.
Jukwaa hilo hilo pia linatumika kusajili vijana kwa mpango wa mafunzo ya kazi ambao Rais aliwahimiza vijana kujiunga nao alipowahutubia katika Uwanja wa Gusii siku ya Alhamisi.
Mradi wa NYOTA umeundwa kushughulikia changamoto nyingi zinazowakumba vijana wasio na ajira kupitia mkakati jumuishi unaohusisha mafunzo, ajira, ujasiriamali na uwekaji akiba.
Serikali inasema kuwa vijana 90,000 watawezeshwa kupata ajira au kuanzisha biashara zao wenyewe kupitia mpango huu, baada ya kufundishwa na kupewa ujuzi unaohitajika.
Kwa vijana wanaochagua kujiajiri, NYOTA hutoa mafunzo ya ujasiriamali yanayochanganywa na mtaji wa kuanzisha biashara.
Wanaonufaika hulazimika kuhudhuria mafunzo ya lazima ya siku nne kuhusu usimamizi wa fedha, ujasiriamali na ukuaji wa biashara kabla ya kupokea fedha.
Mradi huo pia unalenga kujenga ustahimilivu wa kifedha miongoni mwa vijana, huku angalau nusu ya wanufaika wa mpango wa akiba wakitarajiwa kuwa wanawake.
Aidha, NYOTA unawekeza katika kuimarisha mifumo ya kitaifa na ya kaunti ili kusaidia kwa njia endelevu ajira ya vijana na mipango ya uwekaji akiba, huku ukipunguza hatari za upendeleo, uteuzi usio wa haki wa wanufaika na kutengwa kwa makundi fulani.
Ingawa Rais Ruto ameendelea kuandamana na viongozi wa kaunti katika ziara za kugawa fedha hizo, hali ya kisiasa inayozunguka mpango huu imefanya iwe vigumu kwa Wakenya kutenganisha kati ya siasa na uwezeshaji wa kweli wa kiuchumi kwa vijana.