Waliotajwa kwa sakata ya NYS wajiuzulu wasitatize uchunguzi – Mbadi
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano ametakiwa kuwauliza maafisa waliotajwa katika kashfa ambapo Sh9 bilioni zilipotea katika Shirika la Huduma kwa Vijana (NYS) wajiondoe kwa muda ili kutoa nafasi kwa uchunguzi.
Kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa John Mbadi vile vile amewataka maafisa hao kujiuzulu kwa hiari kwa sababu huenda wakatatiza uchunguzi unaoendelea.
Waliotajwa katika sakata hiyo ni Katibu wa Wizara ya Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia Lilian Mbogo, Mkurugenzi Mkuu wa NYS Richard Ndubai na Waziri wa Afya Sicily Kariuki, ambaye aliongoza wizara hiyo mnamo 2016. Ni wakati huo ambapo pesa hizo zilidaiwa kupotea.
“Wito wangu wa kutaka maafisa hawa wakae kando kwa muda haumaanishi kuwa ni wenye hatia. Hofu yangu ni kwamba huenda wakatatiza uchunguzi unaendeshwa na asasi mbalimbali wakati huu,” Bw Mbadi akawaambia wanahabari afisini mwake katika majengo ya bunge.
“Maafisa hao wajiuzulu kwa hiari yao ama Rais Uhuru Kenyatta awalazimishe kukaa kando kwa muda ili kutoa nafasi kwa uchunguzi,” akaongeza Bw Mbadi ambaye pia ni Mbunge wa Suba Kusini.
Kashfa hiyo imekuwa ikichunguzwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na wale wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).
Licha ya madai kuwa ni Sh9 bilioni zilipotea, Bi Mbogo alisema Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imekuwa ikipeleleza kupotea kwa Sh900 milioni wala sio Sh9 bilioni jinsi ilivyoripotiwa katika vyombo vya habari, sakata hiyo ilipofichuliwa juma lililopita.
Alitoa madai hayo kwenye barua aliyomwandikia mkubwa wake Prof Kobia, siku mbili baada Rais Uhuru Kenyatta kumwita ili atoe ufafanuzi kuhusu sakata hiyo ambayo imeipaka tope wizara hiyo kwa mara nyingine.
Katika sakata hii, inadaiwa kuwa maafisa wa NYS walibuni kampuni bandia, na kughushi stakabadhi za zabuni na kutumia udhaifu wa Mfumo wa Ulipaji Fedha Kielektroniki, almaarufu IFMIS, kupora mabilioni ya pesa za umma.
Wakati huo huo, Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma (PAC) imewaita Bi Mbogo, Bw Ndubai na maafisa wengine wa wizara hiyo kuelezea jinsi pesa hizo zilivyopotea.