HabariSiasa

Wanasiasa wanataka kuniua, alia Atwoli

May 6th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

VICTOR OTIENO na JUSTUS OCHIENG

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli amedai kuwa maisha yake yako hatarini. Akiwahutubia wanahabari katika Chuo cha Leba cha Tom Mboya, Kisumu Bw Atwoli alidai kuwa amepokea habari kuwa kuna wanasiasa fulani ambao wamewakodi wahuni ili wamuue katika muda wa wiki moja ijayo.

Bw Atwoli alisema vitisho hivyo vinatokana na matamshi yake kuhusiana na masuala yenye “faida” kwa taifa hili.

“Hivi ni vitisho vya watu wachache ambao wamekodisha majambazi kuniua kwa muda wa wiki moja ijayo. Tayari nimepiga ripoti kwa serikali na nimehakikishiwa kuwa nitalindwa,” akasema Bw Atwoli.

Alipotakiwa kutaja kituo cha polisi ambako amepiga ripoti kuhusu vitisho hivyo, Bw Atwoli alisema: “Nimewaarifu maafisa husika. Vitengo vyote vya usalama vina habari kuhusu mipango hiyo.”

Lakini Msemaji wa Polisi Charles Owino alisema hana habari ikiwa Bw Atwoli amepiga ripoti kwamba maisha yake yako hatarini.

“Sina habari kuhusu ripoti zozote kuhusu vitisho dhidi ya maisha ya Bw Atwoli. Nitawasiliana naye ili anipe ufafanuzi,” akasema Bw Owino, kwa simu.

Atwoli alisema atachukulia suala hilo kwa uzito haswa ikizingatiwa awali vitisho dhidi ya maisha ya viongozi vimepuuzwa ila baadaye wakauawa.

Wakati wa sherehe za Leba Dei Jumanne wiki iliyopita, Bw Atwoli alipendekeza kuwa Katiba ifanyiwe marekebisho ili kubuniwa wadhifa fulani kwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye atastaafu 2022, akisema “Uhuru bado ni kijana sana na akiachwa hivyo atasumbua.”

“Ikiwa hatutarekebisha Katiba, mnadhani Uhuru ataenda wapi na yeye bado ana umri mdogo. Sharti tuirekebishe hiyo Katiba ili tupate nafasi ya kumpa ili asiwasumbue wale ambao watachukua usukani,” akasema katika bustani ya Uhuru, Nairobi.