Habari

WHO yaonya visa vya kisonono sugu vinazidi kupanda

Na HELLEN SHIKANDA November 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RIPOTI mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO) imeonya kuwa ugonjwa wa kisonono unaendelea kuwa sugu kwani ‘hausikii’ dawa zinazotumika kutibu maambukizi hayo ya zinaa.

Ripoti hiyo mpya imechapishwa kupitia mpango wa WHO wa kufuatilia jinsi dawa zimeshindwa kutibu kisonono, ambao hufuatilia kuibuka kwa vimelea visivyotii dawa.

Takriban nchi 12 kutoka kanda tano za WHO ziliwasilisha data mwaka jana, ongezeko la nchi nane ikilinganishwa na 2022.

Visa vilivyoripotiwa kufikia sasa ni takriban 3,615. Kenya haimo miongoni mwa nchi zilizotoa taarifa zake.

Nchi zilizojumuishwa ni Brazil, Cambodia, India, Indonesia, Malawi, Ufilipino, Qatar, Afrika Kusini, Sweden, Thailand, Uganda na Vietnam.

Ripoti inaonyesha kuwa “usafiri wa ndani ya nchi ulihusishwa pakubwa na kuongezeka kwa hali sugu dhidi ya dawa za cefixime, ceftriaxone na azithromycin, ishara kuwa uhamaji unachangia kusambaa kwa vimelea vya kisonono sugu kwa dawa.”

Mkurugenzi wa Idara ya Ukimwi, Kifua Kikuu (TB), Hepatitis na Magonjwa ya Zinaa (STIs) katika WHO, Dkt Tereza Kasaeva, alisema kwamba juhudi za kimataifa zinahitajika kufuatilia, kuzuia na kukabiliana na kisonono sugu ili kulinda afya ya umma duniani.

“WHO inasihi nchi zote kukabiliana na ongezeko la maambukizi ya zinaa na kuingiza ufuatiliaji wa kisonono katika mipango ya kitaifa ya maambukizi ya magonjwa ya zinaa,” alisema.

Uchunguzi unaonyesha kuwa umri wa wastani wa wagonjwa walioonekana kuwa na kisonono sugu ni miaka 27, ingawa waliochunguzwa walikuwa na umri wa kati ya miaka 12 na 94.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 20 ni wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume, huku asilimia 42 wakiripoti kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja ndani ya siku 30 zilizopita. Asilimia nane walitumia dawa karibuni na asilimia 19 walisafiri majuzi.

WHO inasema kuwa kugunduliwa kwa vimelea ambavyo havitibiki kwa dawa zote tatu kuu ni ishara ya dharura ya kuboresha matibabu na kuimarisha ufuatiliaji katika ngazi zote za huduma za afya.

Kanda ya Magharibi ya Pacific ya WHO ndiyo imeendelea kuripoti kiwango cha juu zaidi cha hali sugu dhidi ya dawa zote zilizopimwa.

Kanda za Afrika, Asia ya Kusini Mashariki na Amerika pia zimeripoti viwango vya juu vua dawa ugonjwa kukosa kutibika kwa angalau moja ya dawa zinazotumika.