Habari za Kitaifa

HAMSINI! Watoto wachanga sasa wanalala kaburini kabla ya kuona Kenya mpya waliyopigania!


HAMSINI! Ni idadi ya kutisha ya maafa yaliyonakiliwa Jumanne. Wana na mabinti, kaka na dada, marafiki na wapendwa waliouliwa tangu maandamano ya kupinga serikali ya Kenya Kwanza yaanze mwezi mmoja uliopita.

Maafa mengi yanahusishwa na polisi waliotumia nguvu kupita kiasi walipokabiliana na vijana wengi walioandamana.

Hii ni kulingana na Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu Nchini (KNCHR).

Hamsini. Noti ya shilingi ya Kenya ni nyekundu. Hii ni istiara isiyokusudiwa, ila inachora taswira ya umwagaji damu uliosababishwa na serikali kwa waandamanaji wachanga.

Ni moja ya rangi ya bendera ya kitaifa inayosawiri jinsi wakoloni wna walitesa na kuangamiza Wakenya katika kipindi cha janga la kitaifa kati ya mwaka wa 1950 – 1960.

Hamsini. Kama mtu anaweza kuhesabu kila jina la aliyefariki kulingana na herufi, atakosa herufi mbili tu endapo atahesabu maradufu kutoka A – Z.

Baadhi ya majina, kama yalivyoorodheshwa na Mamlaka Huru ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA), yanahuzunisha.

Rex Kanyike Masai. Evans Kiratu. Ibrahim Kamau Wanjiku. Erickson Kyalo. David Chege. Wilson Sitati. Kelvin Odhiambo Maina. Kenneth Njeru Mwangi. Andrew Mwawasi. Kennedy Onyango.

Kisha kuna jina la Denzel Omondi, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) ambaye aliopolewa kutoka bwawa la Juja, miongoni mwa wengine.

Mwaka wa 1974. Ukipiga hesabu ya miaka 50 kurudi nyuma kwa kila kifo, mwaka huu utakuwa jawabu; ni wakati mwendazake Jomo Kenyatta alikuwa Rais wa Kenya. Huu ni wakati ambapo sakata ya Watergate ilichochea kujiuzulu kwa Rais wa Amerika.

Hamsini, Iwapo wote wangezikwa katika kipande kimoja cha shamba, kila kaburi likisheheni futi 3 kwa 8 za ardhi, bila nafasi kati yao, itahitaji shamba la futi 1,200 mraba — eneo ambalo linaweza kubeba kontena saba na nusu zinazotumika kusafirisha mizigo.

Lakini hapana, hii imekiuka mabehewa ya kusafirisha mizigo. Ni ndoto za watu zilizosafirishwa hadi ulimwengu mwingine.

Ndoto za matuamini zilikatizwa ghafla bila nafasi ya kukata rufaa. Wanafunzi wa chuo kikuu walizikwa ardhini futi sita kabla ya kufuzu. Watu wachanga sasa wanalala chini ya ardhi kabla ya kuona Kenya mpya waliyokuwa wanapigania.

Majeneza ya Wakenya wachanga yalishushwa shimoni yakiwa yamefunikwa na bendera ya Kenya, huku waombolezaji wakigubikwa na ghadhabu.

Idadi hii imekuwa ikipanda tangu Juni 18 wakati vipengele vya Mswada wa Fedha wa 2024 vilikera Wakenya kote nchini.

Katika siku ya kwanza ya maandamano, ilibainika kuwa wengi wa walioghadhabishwa ni Wakenya wa kizazi cha Generation Z (waliozaliwa kuanzia mwaka wa 1997) maarufu Gen Z.

Sasa, maandamano haya yameongeza herufi nyingine. Si tu herufi ‘Z’ ila kuna alfabeti nyingine –‘ L.’ L kusimamia 50 ukizingatia mfumo wa nambari za Kirumi. L inasimamia lawama kwa serikali iliyo’Lala kazini.

Vijana hawa wanaojionea fahari kwa kutokuwa na uongozi walijihami kwa simu, bendera, chupa ya maji na firimbi.

Walirushiwa vitoa machozi walivyozoea na wakazidi kukaza kamba kupigania nchi yao. Hata waliporushiwa maji mazito yaliyowasha, moto wa kupigania haki ulizidi kuwaka ndani yao.

Yamkini, walimotishwa na msemo wa marehemu Martin Luther King Jr, mmoja wa magwiji wa maandamano ya amani, aliyesema kuwa kuna moto ambao hakuna maji yanayoweza kuuzima.

Kisha maandamano yakazaa ‘Vuguvugu la ‘Occupy.’’ Hapa, walinuia kukita kambi katika majengo muhimu ya serikali kama vile bunge la kitaifa na ikulu ili kulilia haki zao.

Walivamia bunge, ikulu na kila mahali. Kwa kweli, walifaulu lakini kadri walipoandamana, ndivyo idadi ya waandamanaji ilizidi kupungua.

Madai ya maandamano kuingiliwa yaliibuka. Ripoti za wahuni kutumwa kufanya maandamano yawe ya uharibifu na wizi zikajiri.

Kila siku ya maandamano ikaanza kuwa siku ya kifo. Visa vya ukatili vikashuhudiwa. Katika maeneo ya katikati ya jiji la Nairobi, Githurai, Rongai… maafa yakazidi kuongezeka. Moja, mbili, tatu, nne, tano….hadi hamsini na bado habari za maafa zinaendelea kutolewa.

Taarifa ya KNCHR Jumanne ilisema watu 21 walifariki Nairobi, Nakuru (3),  Laikipia (2), Narok (1), Kajiado (3), Uasin Gishu (4), Kakamega (2), Kisumu (3), Kisii (1), Mombasa (3), Siaya (1), Kiambi (1), Nandi (1), Embu (1),  Homa Bay (1), Nyeri (1) na Bungoma (1).

Huu si mwisho wa idadi ya vifo kwa sababu milio ya risasi na maafa yaliripotiwa nchini wakati wa maandamano ya Jumanne, Julai 15.

Kitengela, Makueni na Nakuru ni miongoni mwa maeneo ambayo risasi zilifyatuliwa dhidi ya waandamanaji, kwa mujibu wa ripoti.

Shirika hilo la haki ya kibinadamu lilisema litawashtaki wakuu wa huduma ya polisi waliotumia nguvu kupita kiasi.

“Tume hii itahakikisha polisi wanawajibikia matukio ya ukatili yaliyoshuhudiwa,” ilisema taarifa ya KNCHR. “Tunamwomba Rais aheshimu kiapo chake cha kufuata sheria kwa kutoa amri dhidi ya vyombo vya usalama vinavyokiuka haki za binadamu.”

Wizara ya Usalama wa Ndani ilitoa taarifa yenye kichwa “Utakatifu wa maisha ya binadamu lazima uthaminiwe”- taarifa ambayo haikutiwa sahihi.

Anwani yake ingekuwa “Ndiyo, tuliua.” Lakini hiyo ilifichwa ndani ya maandishi hayo ‘yaliyorembeshwa.’

Moja ya aya zake ilisema: “Polisi wanazingatia Sheria ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi ambayo inapinga matumizi ya nguvu kupita kiasi katika utekelezaji wa majukumu yao, lakini Kifungu cha 49 cha Sheria ya Huduma ya Polisi kinawaruhusu maafisa wa usalama kutumia nguvu tu pale inapokuwa lazima na kwa kiwango kinachohitajika katika utekelezaji wa majukumu yao.”

“Mamlaka ya usalama zimeagizwa kuwa waangalifu wakati wa maandamano ya amani na kutotumia nguvu ambayo inaweza kusababisha kifo ili kuhakikishia umma usalama. Polisi wanaweza kuhimizwa kutumia nguvu ya wastani wakati kuna uhalifu kama vurugu, wizi, uteketezaji wa mali, kuvuruga usafiri kwa kuweka vizuizi katika barabara kuu na uvamizi wa miundombinu muhimu na inayolindwa,” iliongeza taarifa hiyo.

Wizara hiyo ilibainisha pia kwamba kile kilichoanza kama pingamizi dhidi ya hali ya uchumi na utozaji ushuru nchini ‘kimegeuka na kuwa hali ya kusikitisha ambapo tunahesabu visa vya watu kupoteza maisha.’

Ndiyo. Watu hamsini wamefariki na bado idadi itapanda. Hamsini inatosha kuunda timu mbili za kandanda kwa mechi ya Kombe la Dunia (yenye wachezaji 23 kila moja, pamoja na wachezaji 11 wa kuanza na wale wa akiba 12). Na bado wachezaji wanne wabaki!

Hamsini. Gari rasmi la Rais William Ruto lina uwezo wa kubeba abiria saba. Ikiwa kila Mkenya aliyefariki angeabiri gari kama hilo, ingehitaji msafara wa magari manane kuwabeba.