Makala

Hivi ndivyo mtu akifariki analipa madeni yake

Na BENSON MATHEKA August 25th, 2024 2 min read

HAKUNA anayejua siku ya kufariki na katika dunia hii, watu huwa na madeni.

Hivyo basi, katika wosia, mtu anaweza kuacha maagizo akieleza  jinsi madeni yake, ukiwemo ushuru, yanapaswa kulipwa au kushughulikiwa.

Katika wosia, sio lazima anayeuandika ateue au kutaja mtekelezaji wa wosia wake.

Akifanya hivyo ni kwa hiari yake lakini hakuna hitaji la kisheria kumlazimisha mtu kufanya hivyo.

Pale ambapo mtekelezaji wa wosia anakosa kuteuliwa, warithi watarajiwa wanaweza kwenda kortini na kuomba kibali cha kusimamia mali yake.

Familia zikubaliane

Ni muhimu kwa familia kukubaliana mtu au watu wa kusimamia mali ya marehemu ili kuepuka mizozo kabla ya kwenda kortini kuomba kibali.

Msimamizi huwa anasimamia mali kwa niaba ya warithi watarajiwa wengi kusubiri mchakato wa kuigawa kulingana na wosia wa marehemu.

Tatu, japo sio hitaji la lazima la kisheria, mtu anayeandika wosia anaweza kuteua walezi au waelekezi wa watoto wake walio na umri mdogo.

Kisheria, kila mtu aliye na umri wa chini ya miaka 18 ni mtoto.

Mahitaji ya kisheria

Hata hivyo anayeteuliwa anapaswa kutimiza mahitaji ya kisheria ikiwa ni pamoja na uadilifu katika kutunza na kuhifadhi mali wanayoachiwa watoto na marehemu.

Ni muhimu nieleze kuwa sehemu za wosia wa mtu zinaweza kubatilishwa na korti iwapo itaridhika kuwa zilikiuka sheria.

Kwa mfano, ikibainika kuwa marehemu aliachia mtu mali isiyokuwa yake, basi mali hiyo haiwezi kutwaliwa na anayedaiwa kurithishwa.

Nataka kufafanua kuwa ni sehemu ya wosia inayothibitishwa kuwa kinyume cha sheria inayoweza kubatilishwa na si wosia wote. Hata hivyo, korti ina nguvu za kubadilisha maudhui ya wosia ikihisi kuna sababu za kufanya hivyo.

Kwa mfano, korti ikithibitishiwa kuwa mtu aliyekuwa akitegemea marehemu hakuachiwa mali ya kutosha kufadhili maisha yake na mali hiyo iwepo, inaweza kuagiza anufaike na mali zaidi  ya marehemu. Iwapo marehemu aliteua mtekelezaji wa wosia wake, ni lazima apate idhini ya korti kabla ya kufanya hivyo.

Hii huwa ni ya kuthibitisha jukumu alilotwikwa na marehemu.

Kwa hivyo mtu hawezi kuamua kutekeleza wosia wa mtu kiholela japo sio hitaji la kisheria kwa mtu kutaja mtekelezaji wa wosoa. Anapofanya hivyo, lazima anayetwikwa jukumu hilo apate idhini ya korti.