Habari za Kitaifa

IEBC kupiga mnada mali ya wanasiasa waliolemewa na kesi za uchaguzi 

Na DAVID MWERE August 28th, 2024 2 min read

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeanza mchakato wa kutafuta madalali kuisaidia kukomboa Sh400 milioni kutoka kwa wanasiasa walioamriwa na korti kuilipa gharama ya kesi walizowasilisha kulalamikia matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita, 2023.

Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC, Bw Marjan Hussein Marjan, alifichua mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Umma kwamba tume iliamua kutumia madalali baada ya kupata idhini kutoka kwa Afisi ya Mwanasheria Mkuu.

Hii ilikuwa baada ya mawakili waliotwikwa jukumu la kufuatilia pesa hizo kutoka kwa wanasiasa kupata vizingiti, ikiwa ni pamoja na kushindwa kupata dhamana iliyowekwa katika kesi za uchaguzi na gharama ya kufuatilia malipo hayo.

“Kwa sasa tunaendelea na mchakato wa kutafuta madalali kupata pesa ambazo tume inadai ambazo ilitunukiwa na korti katika kesi za uchaguzi ambazo ilishinda,” Bw Marjan aliambia kamati.

Changamoto nyingine ambayo mawakili walikumbana nayo ni kucheleweshwa kwa utekelezaji na kusimamishwa kwa maagizo ya utekelezaji na walalamishi.

Aidha, kuna watu wanaowasilisha kesi kwa niaba ya wanasaisa ili kuwakinga dhidi ya gharama ya kesi na kutokuwepo kwa orodha ya madalali waliotambuliwa kufuatilia malipo hayo.

Madalali hao, Bw Marjan alihakikishia kamati, watalipwa asilimia ya pesa watakazokusanya ambayo ni “asilimia 1.5.”

“Tumetumia juhudi nyingi kupata pesa hizo lakini hatujafaulu. Hii ndiyo sababu tumeamua kutumia madalali kwa ushauri wa Mwanasheria Mkuu,” Bw Marjan alisema.

Alisema kuwa kati ya Sh400 milioni ambazo tume inadai wanasiasa, mawakili waliweza kupata Sh6.8 milioni pekee kutoka kwa walalamishi walioshindwa katika kesi za uchaguzi.

“Tume inapaswa kuwa na orodha ya madalali kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi na Uuzaji wa Mali ya Umma 2015, kutekeleza maagizo kadhaa yanayohusu ushuru,” aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi alisema akishauri tume.

Bi Dorcas Oduor ndiye amemrithi aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi wakati huo, kufuatia mabadiliko ya Baraza la Maziri aliyofanya Rais William Ruto majuzi.

Bw Muturi alikuwa akijibu barua ambayo aliandikiwa na Bw Marjan Februari 8, 2023 akielezea matatizo ya tume ikijitahidi kufuatilia pesa hizo.

Walalamishi ambao tayari wamelipa tume Sh6.8 milioni, ni pamoja na chama cha Party of Independent Candidates of Kenya (PICK) kinachohusishwa na aliyekuwa mbunge wa Kilome John Harun Mwau (Sh2.23 milioni), aliyekuwa mbunge wa Gatundu Kaskazini MP Waibara (Sh333, 333), Bw Arthur Kibira Sh300, 000 na Bw Mugambi Imanyara Sh250, 000.

Wengine ni aliyekuwa Waziri John Munyes (Sh250, 000), Bi Grace Akumu (Sh250, 000), Bi Pauline Lokuruka (Sh250, 000), Hamzah Kevogo (Sh250, 000), Bw Robinson Simiyu (Sh250, 000) na Bw Charles Kamuren Sh250, 000.

Tume inasema kwamba imekuwa vigumu kupata pesa hizo kutoka kwa wanasiasa husika kwa sababu ya kukabiliwa na changamoto kadha wa kadha, ikiwemo kushindwa kupata baadhi yao huku wengine wakiwa hawana mali inayojulikana inayoweza kupigwa mnada.