Habari za Kitaifa

KDF yapoteza ardhi iliyojenga kambi, mahakama ikisema sheria haikufuatwa

Na JACOB WALTER July 21st, 2024 1 min read

JESHI la Ulinzi la Kenya (KDF) limepoteza takriban ekari 2,500 za ardhi ambayo kuna kambi ya kijeshi katika eneo la Karare baada ya Mahakama Kuu ya Isiolo kuamua kwamba ardhi hiyo ilitwaliwa kinyume cha sheria.

Katika uamuzi ambao ulitolewa na Jaji mkazi Peter Muchoki Njoroge akisaidiwa na wengine wawili, Mahakama Kuu ilibainisha kuwa KDF ilikosa kufuata kikatiba na kisheria za utwaaji ardhi.

“Baada ya kupitia kwa makini wasilisho lililoletwa mbele ya mahakama hii, tungependa kusema kwamba hatuwezi kushawishiwa kusafisha makosa,” Jaji Njoroge alisema.

Kwa hivyo, Mahakama Kuu iliamuru serikali ya kitaifa na kaunti kulipa jamii zilizoathiriwa Sh30 milioni zitakazotolewa kama gharama ya kesi kuanzia 2020.

Pesa hizo zitaelekezwa katika kukuza miradi ya maendeleo ya jamii na kuwa chini ya usimamizi wa Mdhamini anayejumuisha MCA wa eneo, mwakilishi kutoka afisi ya kamishna wa kaunti, mwakilishi kutoka serikali ya kaunti na wawakilishi wawili kutoka wa mlalamishi wa kwanza, wa pili na wa tatu.

Katika mawasilisho, mahakama ilielezwa kuwa mnamo 2019, KDF ilionyesha nia ya kupata angalau ekari 2,500 za ardhi katika kaunti ndogo ya Saku, Kaunti ya Marsabit.

KDF ilipoenda kwa jamii za Rendille na Samburu, ilielekezwa kwenye ardhi katika maeneo ya Kubi Kalo na Mata Lama ambayo iliikataa lakini ikatwaa eneo hilo kwa nguvu.

Jamii zilipendekeza ardhi mbadala kwa KDF kwa kuzingatia mambo kama vile uendelevu wa mazingira, maadili ya kitamaduni, usawa, na athari kwa chakula na hatari za umaskini uliokithiri.

KDF iliingia na tingatinga kwenye ardhi iliyozozaniwa mnamo Mei 29, 2020, licha ya pingamizi na maandamano ya jamii.

Kulingana na mahakama, ardhi hiyo ilikuwa sehemu ya kilomita 877.30 mraba inayotegemewa na wakazi wasiopungua 200,000.

Eneo hilo lilitegemewa na jamii za wafugaji wanaoishi Karare, Songa, Loglogo, Kamboye, Laisamis, Kargi na Korr.

Majaji walisema kwamba hakukuwa na ushirikishaji wa umma katika utwaaji wa ardhi hiyo.