Akili Mali

Ajabu ya bei kushuka Oktoba lakini bidhaa muhimu kama nyama, mafuta, machungwa zikipaa

Na BENSON MATHEKA November 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAKENYA walipata afueni baada ya mfumko wa bei kupungua kwa asilimia 2.7 mwezi uliopita wa Oktoba 2024, kutoka asilimia 6.9 katika kipindi hicho mwaka jana.

Data kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu Kenya (KNBS), zinaonyesha kuwa kiwango cha mfumko wa bei kwa mwezi pia kilishuka hadi asilimia 3.6 Oktoba 2024.

KNBS inahusisha kushuka kwa mfumko na kupungua kwa gharama ya usafirishaji wa bidhaa, bei za vyakula na vinywaji visivyo na kileo, nyumba, maji, umeme, gesi na mafuta.

Bei za unga wa mahindi, unga wa ngano, sukuma wiki, petroli na dizeli zilipungua kidogo Oktoba. Hata hivyo, licha ya mfumko wa bei kupungua, baadhi ya bidhaa muhimu zilipanda bei mwezi wa Oktoba.

KNBS inasema mafuta ya kupikia, nyama ya ng’ombe, nyanya, machungwa, karoti na maembe zilipanda bei kwa kiasi kikubwa mwezi Oktoba ikilinganishwa na Septemba.

Bei ya maembe, karoti, machungwa na nyanya ilipanda kwa asilimia 9.9, asilimia 5.7, asilimia 5.1 na asilimia 3.7 mtawalia. Bei ya sukari na unga wa mahindi ilipungua kwa asilimia 2.3, 1.8 na 1.7 mtawalia kati ya Septemba 2024 na Oktoba 2024, inasema ripoti ya KNBS.

Inaeleza kuwa, maji, stima, gesi na mafuta ilishuka kwa asilimia 0.3 kati ya Septemba 2024 na Oktoba 2024 kutokana na kupungua kwa bei ya mafuta ya taa na gesi ya LPG kwa asilimia 4.3 na asilimia 0.4 mtawalia.

Katika kipindi hicho, hata hivyo, bei za kilowati 50 za umeme na kilowati 200 za umeme ziliongezeka kwa asilimia 0.3 na asilimia 0.2, mtawalia.

Tangazo hilo la KNBS linajiri wakati serikali inalenga kiwango cha mfumko wa bei cha kati ya asilimia 2.25 na 7.5 katika muda wa kati.

Gharama ya usafiri, kulingana na KNBS, ilipungua kwa asilimia 0.3 kati ya Septemba na Oktoba 2024. Hii, shirika linaeleza, ilichangiwa zaidi na kupungua kwa bei ya petroli na dizeli kwa asilimia 4.3 na asilimia 2.0 mtawalia.

Mapema mwezi huu, Benki Kuu ya Kenya (CBK) ilipunguza kiwango chake cha mikopo kwa asilimia 0.25 kutokana na kushuka kwa mfumko wa bei katika miezi ya hivi majuzi.