Gavana Wanga apendekeza Ruto aalike Arsenal 2026 ichuane na Harambee Stars kwa heshima za Raila Odinga
GAVANA wa Homa Bay, Gladys Wanga amependekeza mwaka ujao, 2026 klabu ya Arsenal ialikwe ili itoane kijasho na timu ya Kenya, Harambee Stars kama njia ya kumheshimu Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga anayezikwa leo, Jumapili, Oktoba 19, 2025.
Bi Wanga, ambaye pia ni mwenyekiti wa ODM, chama kilichoongozwa na Bw Raila, ametoa ombi hilo kwa Rais William Ruto anayeoongoza hafla ya mazishi ya mwendazake nyumbani kwake Bondo, Kaunti ya Siaya.
Akitoa pendekezo hilo, Gavana Wanga amesema kualika Arsenal imenyane na Harambee Stars ni heshima kwa Bw Raila – ambaye alikuwa mfuasi sugu wa timu hizo mbili.
“Baba (akiashiria Raila Odinga) alikuwa shabiki wa Arsenal na ODM, na sikujua hata wewe Rais ni mfuasi wa Arsenal. Hivyo, tunakuomba 2026 ualike Arsenal icheze na Harambee Stars, kwa heshima za Raila ambaye alikuwa shabiki wa timu hizo mbili,” Bi Wanga akasema.
Hali kadhalika, Gavana huyo anapendekeza uga wa kisasa wa Talanta unaoendelea kuundwa Nairobi upewe jina la Raila Odinga.
“Uwanja wa Talanta ukimalizika upewe jina la Raila Odinga Talanta Stadium, na Arsenal na Harambee Stars wachezee humo mwaka ujao.”