Makala

Hofu watoto wengi wakiacha shule kufanya kazi katika mashamba ya miraa Meru

Na DAVID MUCHUI December 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WASIWASI umetanda katika eneo la Igembe, Kaunti ya Meru baada ya kubainika kuwa watoto wapatao 30.000 wanafanya kazi katika mashamba ya miraa.

Na sasa wazee wa jamii hiyo wameingilia kati kuokoa watoto hao.

Watoto hao huanza kufanya kazi katika mashamba ya miraa wakiwa na umri wa miaka 10 na kuwafanya wakose fursa ya kusoma.

Malipo hutegemea aina ya mmea huo ambapo mchumaji miraa anaweza kutia mfukoni hadi Sh 1,000 kwa siku.

Watoto hawa wanakumbwa na visa vya unyanyasaji na kupunjwa na watu wazima ambao huwalipa malipo ya chini.

Hali ya wasiwasi imegubika wakazi kufuatia idadi kubwa ya watoto wanaohusishwa na kazi ngumu,

Kulingana na takwimu zilizokusanywa kwa usaidizi wa uongozi wa mtaa, zaidi ya watoto 30,000 maeneo ya Igembe Kaskazini, Igembe Kusini na Igembe ya Kati hawahudhurii shule.

Takwimu za sensa ya 2019 zilibaini kuwa Kaunti ya Meru ndiyo kaunti yenye asilimia kubwa zaidi (asilimia 18) ya wanafunzi wanaoacha shule katika kiwango cha shule ya msingi.

Bw Peter Ntoitha, mzee wa Njuri Ncheke, amesema baraza la wazee lina mpango wa kupiga marufuku utafunaji miraa kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18.

“Kama wazee, tumegundua suala la watoto kuacha shule limekita mizizi eneo la Igembe. Tumeelewana na polisi na machifu kuchukua hatua kuzuia watoto walioacha shule kufanya kazi katika mashamba ya miraa na mijini. Lazima tuokoe kizazi chetu ambacho ni changa,” akasema Bw Ntoitha.

Katibu wa Njuri Ncheke tawi la Igembe Kusini Frederick Limiri alisema wamegundua wazazi wanazidi kuwatelekeza watoto wao na kuwalazimisha kufanya kazi.

“Wazazi wanapokosa kutimiza mahitaji ya watoto wao, huwabidi kutafuta kazi ili wajisaidie,” alisema Bw Limiri.

Kulingana na Jennifer Kathure, wamiliki wa mashamba hupendelea watoto kufanya kazi kwa sababu ya malipo ya chini.

“Watoto ndio wafanyakazi bora kwa kuwa ni wepesi wanapochuna miraa, kwa hivyo hawaharibu mazao,” akasema.

Imebainika kuwa wavulana hao huishia kufanya biashara za bodaboda.

“Uvunaji na upakiaji wa miraa hufanywa kwa saa chache tu. Kwa hivyo wavulana hawa hutumia muda mwingine uliobaki katika kazi za usafiri wa bodaboda,” alisema Bw Joseph Mutia, Mshirikishi wa Mipango katika shirika la Kangaroo Community Care Kenya.

Shirika hili hushughulikia urekebishaji wa mienendo ya watoto wanaofanyishwa kazi.

Imetafsiriwa na Labaan Shabaan