KINAYA: Mkenya mwenzangu, kelele unazosikia kila kona ni za fisi wanaokutamani kama mpiga kura!
UNATAMBUA kuwa mtu ni muongo anapokuapia Jalali eti hajawahi kumuua hata sisimizi. Sote tumewaua sisimizi aisee!
Si kimakusudi, lakini ukweli ni kwamba sote tumewaua. Ama umetenda dhambi hiyo ukitembea peku au kwa msaada wa viatu, umemkanyaga kiumbe huyo katika pitapita zako.
Wala hujawahi kusimama na kuomba msamaha au angaa kujutia kosa lako. Hujali! Sisimizi hana thamani, akifa kuna nini?
Na, kama muuaji wa kawaida tu, umekataa kamwe kuhudhuria mazishi ya sisimizi na wadudu wengine wadogo ambao wewe mwenyewe umewahi kuwatoa uhai.
Usithubutu kuniuliza eti mazishi ya sisimizi huhudhuriwaje! Wanasayansi wangependa wangetusaidia kwa hilo, lakini hata nao pia ni wauaji wasio na utashi wa kurekebisha au kuwajibikia makosa yao.
Watu walio na muda wa kutosha kuchunguza maisha ya nzi, mpaka wakajua hawaishi kwa muda wa zaidi ya wiki moja, wakitaka watakwambia misiba ya wadudu wote hufanyikaje.
Kuambizana ukweli ni kwetu sisi kukubali, japo kimoyomoyo, kwamba tumewaua sisimizi na wadudu wengineo, si kukanusha kosa hilo kadamnasi ya watu. Tuwe wangwana.
Mama jirani, Samia Suluhu Hassan – baada ya Watanzania jasiri kumjia juu kutokana na visa vingi tu vya watu kutoweka na wengine kuuawa na kutupwa mitoni na baharini – amekanusha kumuua hata sisimizi akaambiwa ‘ngoja Mama’!
Nawavulia kofia Watanzania kwa kuanza kupevuka kisiasa, sikwambii na kulikabili dola ambalo limejitekea na kujiulia kila linayetaka kwa raha na wepesi wa kupigiwa mfano.
Wamemwambia Mama kuwa kila mwakilishi wa dola anayetenda kosa au kazi nzuri anafanya hivyo kama mwakilishi wa serikali kuu, na msimamizi wa serikali hiyo ni Mama mwenyewe.
Kwa ufupi, kwa raha na shida, Mama hawezi kujitenga na kila kinachofanyika nchini mwake. Serikali ni yake, amenunua utumbo, aache kuwaogopa nzi.
Ameambiwa ikiwa anakubali kusifiwa madarasa yakijengwa vijijini, basi na akubali kwamba maiti wanaoelea mitoni na baharini ni kazi ya mikono yake.
Simlaumu kwa kukimbia lawama. Ni hulka ya wanasiasa kutaka sifa nzuri pekee, mbaya ziwaendee wapinzani. Hata ni heri Tanzania ambayo ina upinzani.
Huku kwetu Kenya, wapinzani wanapigania ukewenza, kila mmoja akitaka kuwasadikisha wenzake kwamba ndiye anayependwa zaidi. Yupo pia mtalaka, Riggy G, anayetukana kila mtu kwa kuwa ndoa yake ilivunjika, na hakuna kurudiana!
Tumeachiwa fundi mjua yote, mcheza ngoma akaicheza kwa makalio! Kasongo amekakamaa hivi kwamba tukiteta kuhusu utekaji nyara unaoendelea nchini anatwambia ‘tutaacha mambo hayo’.
Ama hajali kwamba anakiri kosa baya, akidhani hakuna chochote unachoweza kumfanyia kwa kuwa wake zake watakumeza mzima-mzima, au anafikiri huna akili za kutosha kugundua kuwa amekiri kosa.
Mwenzangu, hata ukiona ugumu, lazima utumie akili ili usalie hai. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alituasa kuwa mnyama anayeonja nyama ya binadamu anajua ina ladha ya chumvi, hivyo haachi kuitamani. Kumbuka nyama yako tamu, fisi hahitaji kukukaanga.