Jamvi La Siasa

Mlima bado telezi licha ya mapokezi ya Ruto

Na  MACHARIA GAITHO April 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

WANAMIKAKATI wa kisiasa wa Rais William Ruto wana kila sababu ya kufurahia matokeo ya ziara yake katika eneo la Mlima Kenya kwa kuwa wakazi walijitokeza kwa wingi kumsikiliza na kumshangilia alipozuru maeneo mbalimbali ya ukanda huo.

Hofu kwamba kampeni hiyo iliyopewa jina la ziara ya ‘maendeleo’ ingepuuzwa au hata uhasama wa moja kwa moja, hasa kutokana na kauli za mara kwa mara za “Ruto lazima aondoke” ilibainika kuwa si ya kweli kwa kuwa ziara hiyo iliendelea bila matukio makubwa, isipokuwa kuzomwa kwa baadhi ya wabunge wa eneo hilo, na wala si Rais mwenyewe.

Kwa wafuasi wa Rais Ruto, ziara hiyo ilikuwa ushindi mkubwa dhidi ya dhana kwamba, alikuwa amepoteza kabisa ushawishi katika Mlima Kenya kufuatia kuondolewa mamlakani kwa Rigathi Gachagua mwaka jana.

Mapokezi mazuri yanaibua maswali kuhusu madai ya Gachagua kuwa yeye ndiye mwelekezi wa kura za Mlima Kenya na ndiye atakayeamua mwelekeo wa kisiasa wa eneo hilo kuelekea uchaguzi wa 2027.

Iwapo ziara hiyo ilikuwa kama mashindano ya nani ni “Mfalme wa Mlima” kati ya Rais na naibu wake aliyeondolewa madarakani, basi Ruto alikuwa mshindi wa wazi kufikia mwisho wa ziara hiyo.

Lakini hilo lilikuwa ni pambano la kwanza tu katika msururu wa vita vya kisiasa vinavyotarajiwa kufuata.Wafuasi wa Gachagua wanaweza kujifariji kwa kusema kwamba kushangiliwa na umati si kipimo halisi cha mwelekeo wa kisiasa.

Watadai pia kuwa waliepuka makabiliano kwa makusudi.Jambo moja lililoleta mafanikio makubwa ni upangaji wa kina na rasilimali zilizotumika kuhakikisha ziara hiyo ilifaulu.

Wiki kadhaa za maandalizi zilihusisha mikutano ya wabunge, magavana na viongozi wengine wa eneo hilo, pamoja na mawaziri, makatibu, wakuu wa mashirika ya serikali, na maafisa wakuu wa usalama waliowekwa kuhakikisha umati mkubwa ulishuhudiwa na kuzuia vurugu.

Gachagua alitazama ziara hiyo kwa mbali, kinyume na kauli zake za awali kuwa Ruto hangeruhusiwa kukanyaga Mlima Kenya. Kauli yake ya pekee kabla ya ziara ilikuwa kuwahimiza wananchi wakubali pesa watakazopewa kuhudhuria mikutano, akisema ni kodi yao wanayorudishiwa, akiashiria kuwa pesa nyingi zilitengwa “kukodisha umati”.

Kauli yake nyingine ilikuwa kupuuzilia mbali madai ya Ruto katika mahojiano na vyombo vya habari vya eneo hilo kwamba Gachagua alitaka Sh 10 bilioni ili aendelee kumuunga mkono kuelekea uchaguzi wa 2027.

Kwamba Ruto alifanya mahojiano hayo na kutoa madai mazito, ingawa hayakuthibitishwa, ni dalili kuwa Ruto aliipa ziara ya Mlima Kenya uzito mkubwa. Huenda hakuwahi kuwekeza rasilimali na muda mwingi kwa ziara yoyote kama hiyo katika sehemu nyingine ya Kenya.

Iwapo hivi vilikuwa ni vita vya kugombea “moyo na roho” ya Mlima Kenya, basi ilikuwa fursa muhimu kwa Ruto kudhihirisha kuwa hajakubali kushindwa na naibu wake wa zamani.

Kufuatia kujiondoa kwa Gachagua katika mrengo wa Ruto, wengi walidhani kuwa nafasi ya Ruto kuchaguliwa tena ilikuwa imepungua sana.Ruto alijibu hali hiyo kwa kuingia katika makubaliano ya kisiasa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, ambaye ana ufuasi mkubwa ambao ungetumika kufidia kura za Mlima Kenya.

Baada ya makubaliano hayo, kulikuwa na ishara kwamba Ruto alikuwa tayari kuachana na kura za Mlima Kenya na kujenga ushirikiano mwingine.Washirika wa Raila katika serikali jumuishi” walianza kusukuma ajenda inayofanana na ile ya “41 dhidi ya 1” ya mwaka 2007, iliyolenga kuunganisha jamii nyingine dhidi ya kura za Mlima Kenya.

Mbunge wa Homa Bay Peter Kaluma alieleza wazi kuwa lengo la muungano wa Ruto-Raila ni kuhakikisha Mlima Kenya umetengwa kwa madai kuwa wamepata zaidi ya walivyostahili kutoka kwa serikali zilizopita.

Mawaziri wapya kutoka ODM kama John Mbadi (Hazina), Opiyo Wandayi (Nishati), na Ali Hassan Joho (Madini) waliashiria kwamba rasilimali za maendeleo zielekezwe Nyanza, Pwani na maeneo mengine yaliyosahaulika.

Hata kulikuwa na wito wa mabadiliko makubwa serikalini, ambapo mawaziri na maafisa wakuu wanaohusishwa na Gachagua wangetolewa na nafasi zao kuchukuliwa na watu kutoka maeneo mengine.

Wakati huo huo, Ruto alimwendea Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kuwasilisha majina ya watu wa kuteuliwa serikalini. Ingawa Uhuru alikataa, alisema hakuwa na tatizo Ruto akiteua watu kutoka Mlima Kenya. Hivyo ndivyo Mutahi Kagwe (Kilimo), Lee Kinyanjui (Biashara), na William Kabogo (ICT) walivyoingia kwenye baraza la mawaziri.

Ruto alisambaza ujumbe kwamba walioteuliwa walikuwa watu wa Uhuru, ingawa uhusiano wao pekee u ni asili yao ya Mlima Kenya.Dhamira ilikuwa kuonyesha kwamba Uhuru pia anaiunga mkono serikali ya mseto, na pia kupunguza nguvu ya Gachagua kwa kutumia tofauti zake na Uhuru kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa Mlima.

Lakini kipimo halisi kilikuwa ni mapokezi ya Ruto mwenyewe katika Mlima Kenya – jambo ambalo kwa kiasi fulani lilifanikiwa.Tofauti na ngome ya Raila huko Nyanza, wapiga kura wa Mlima Kenya si wafuasi wa mtu mmoja tu.

Hawakumfuata Hayati Rais Mstaafu Kibaki mwaka 2013, wala hawakumtii Uhuru alipojaribu kumpigia debe Raila mwaka 2022.Kuelekea uchaguzi wa 2027, Gachagua anaweza kupoteza ushawishi ikiwa hatadhihirisha anaweza kuwaongoza watu wake hadi ‘nchi ya ahadi’.

Lakini changamoto ni kwamba iwapo hatashinda kesi yake ya kuondolewa kama Naibu Rais, hataweza kugombea urais.Gachagua anaelewa hilo, na pia anajua kuwa kumsimamisha mgombea mwingine kutoka Mlima Kenya huenda si busara wakati taifa limechoshwa na uongozi wa kurudiarudia kutoka jamii hiyo.