Ndoa ya Raila na Ruto sasa tishio kwa uhuru wa IEBC
NDOA ya kisiasa ya kati ya Rais William Ruto na Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, imeanza kutishia kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) huku kiongozi wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, akiibua wasiwasi kuhusu uadilifu wa mchakato huo.
Japo mchakato huo umepiga hatua na ni vigumu kuusitisha, Kalonzo asema ukuruba wa kisiasa wa Rais Ruto na Bw Odinga unaweza kufanya Wakenya kukosa imani na tume itakayoundwa.
Kalonzo anadai ushirikiano wa kisiasa kati ya Rais Ruto na Odinga, unahatarisha mchakato wa kuunda IEBC iliyo huru. Katika barua yake kwa viongozi hao wawili, Kalonzo alisisitiza kuwa IEBC inapaswa kuundwa kwa njia shirikishi ili kuhakikisha uchaguzi wa 2027 unakuwa huru, wa haki, na wa kuaminika.
Kwa mujibu wa Kalonzo, makubaliano ya kisiasa kati ya Chama cha United Democratic Alliance (UDA) na Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) yanahujumu nafasi ya upinzani katika mchakato wa kuunda IEBC.
Tangu vyama hivi viwili vilipotia saini Mkataba wa Maelewano (MoU) hadharani katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta (KICC) mnamo Machi 7, 2025, imekuwa dhahiri kwamba ODM na UDA wanashirikiana.
Makamu rais huyo wa zamani aliandika barua hiyo Machi 21 mwaka huu huku wandani wake wakifichua kuwa hofu ya upinzani inatokana na hisia kuwa marafiki wengi wa Ruto na Raila wanamezea mate nyadhifa za mwenyekiti na makamishna wa IEBC.
Kalonzo asema kuwa ikiwa ODM na UDA zitaendelea kusukuma ajenda ya kuunda IEBC bila kushirikisha upinzani, basi itakuwa wazi kuwa serikali inapanga kuunda tume ya uchaguzi yenye upendeleo.
“Kama taifa, hatuwezi kuruhusu historia ya uchaguzi wenye utata kujirudia. Hatutakubali IEBC iwe chombo cha maslahi ya kisiasa ya upande mmoja,” alisema Kalonzo.
Katika barua yake, Kalonzo asema kuwa UDA na ODM, ambavyo sasa ni washirika wa kisiasa, vinapaswa kushirikiana na upinzani ili kuhakikisha kwamba mchakato wa kuunda IEBC unakuwa wa haki na wa wazi.Akiendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano, Kalonzo alionya kuwa kutoshirikisha upinzani katika mchakato huu kutasababisha mgawanyiko mkubwa wa kisiasa na kuhatarisha uthabiti wa taifa.
Mbali na hayo, Kalonzo alitahadharisha kuwa ikiwa UDA na ODM zitaendelea na uteuzi wa mwenyekiti wa IEBC na makamishna wake bila ushiriki wa maana wa upinzani, basi hatua hiyo itachukuliwa kama jaribio la kupanga udanganyifu wa uchaguzi wa 2027 mapema.
“Tunajua madhara ya uchaguzi uliojaa dosari. Kama viongozi wa upinzani, hatutakubali njama zozote za kuhujumu demokrasia na haki ya wananchi kuchagua viongozi wao kwa njia huru na haki,” alisema.
Kalonzo alisisitiza kuwa kwa maslahi ya taifa, Ruto na Raila wanapaswa kufanya jambo sahihi kwa kushirikisha upinzani katika mchakato wa kuunda IEBC. Kwa sasa, macho yote yameelekezwa kwa Rais Ruto na Raila Odinga kuona iwapo watazingatia wito wa Kalonzo au wataendelea na mkakati wao wa kisiasa unaoonekana kutenga upinzani katika maamuzi muhimu ya taifa.
Kwa mujibu wa wachanganuzi wa siasa, barua ya Kalonzo inaonyesha ukuraba wa Rais Ruto na Bw Odinga unawatia baridi vinara wa upinzani hata kabla ya wao kuungana rasmi.
“Ina mantiki kwa upande mmoja na kwa upande mwingine inaonyesha wazi kuwa vinara wa upinzani, ambao kufikia sasa hawajaungana rasmi, wameingiwa na baridi mapema. Mantiki nayo ni kwamba, uteuzi wa wanachama wa jopo la kuteua mwenyekiti na makamishna wapya wa IEBC ulishawishiwa zaidi na Raila na Ruto.Baridi inatokana na uhalisia kwamba wawili hao wanaweza kuweka vibaraka wao kuwapendelea katika uchaguzi mkuu wa 2027,” asema mdadisi wa siasa Mike Kariuki.
Hata hivyo, anasema jinsi hali ilivyo, ni vigumu kusitisha mchakato unaoendelea wa kuunda IEBC na Kalonzo na wenzake watalaumiwa kwa kutaka kuyumbisha shughuli hiyo muhimu katika maandalizi ya uchaguzi.