Jamvi La Siasa

Uchanganuzi: Azma ya Waiguru 2027 ni mwiba kwa Gachagua Mlimani

Na BENSON MATHEKA August 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

GAVANA wa Kirinyaga Anne Waiguru atakuwa mwiba kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua eneo la Mlima Kenya iwapo ataamua kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Viongozi wanawake waliokutana Machakos kwa siku mbili wiki hii walimshinikiza waziri huyo wa zamani kugombea urais baada ya kukamilisha muhula wake wa pili kama gavana 2027.

Wachanganuzi wa siasa wanasema ikizingatiwa kuna mgawanyiko mkubwa katika eneo la Mlima Kenya ikiwemo vitisho vya kumtimua Gachagua ofisini, huenda wito wa Waiguru kugombea urais ukaongeza masaibu ya naibu rais kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

“Waiguru amekuwa akijiandaa kwa wadhifa mkubwa na yaliyofanyika Machakos ambapo viongozi wanawake kutoka nje ya Mlima Kenya walionekana kumwidhinisha ni miongoni mwa mikakati yake. Ilinuiwa kuonyesha ana ushawishi kitaifa,” asema mchambuzi wa siasa Daisy Muhia.

Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani na aliyekuwa Gavana wa Kitui Charity Ngilu, walimpigia debe Bi Waiguru wakisema anatosha kuwa kiongozi wa nchi hii.

Katika kauli iliyoashiria kukubali himizo hilo, Bi Waiguru alijibu: ‘Mungu ajibu maombi hayo,’ Bi Waiguru.

Kulingana na Muhia, kujitosa kwa Waiguru katika kinyang’anyiro cha urais ni pigo kwa Gachagua ambaye anapambana kuonekana kuwa msemaji wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya.

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Magavana amewahi kumkosoa Gachagua kwa kile alichodai kuwa hulka ya naibu rais ya kuzima azima za viongozi wanaomezea mate nyadhifa za juu serikalini.

“Japo tunaheshimu Afisi ya Naibu Rais, na afisi nyingine yoyote ya uongozi, demokrasia endelevu haituruhusu tunaoshikilia afisi za uongozi za umma kuzichukulia kama mali ya kibinafsi kiasi kwamba ni mwiko kwa mtu mwingine yeyote kueleza azma yake,” Waiguru alisema Mei 20 mwaka huu akijibu Gachagua aliyelaumu baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya kwa kuzua migawanyiko.

‘Tunashikilia afisi hizi kwa uaminifu si kama wamiliki. Tutambue haki ya wote, hasa wanawake wetu na vijana wetu kutamani vyeo vya juu,’ aliongeza.

Kulingana na wadadisi wa siasa, Waiguru amekuwa akijipanga na hata kama hatagombea urais lengo lake ni kubaki katika siasa.

“Jina lake limekuwa likitajwa miongoni mwa wanaoweza kuwa wagombea wenza wa Rais William Ruto iwapo ndoa ya kiongozi wa nchi na Gachagua itazama kabla au katika uchaguzi mkuu wa 2027. Hii ni iwapo rais ataamua kuendeleza ukuruba wake na eneo la Mlima Kenya,” akasema mchambuzi wa siasa Meshack Njenga.

Anasema wito wa viongozi wanawake wa kumuunga Waiguru kugombea urais una uwezo wa kuvuruga hesabu ya Gachagua ya kujijenga kama msemaji wa kisiasa wa eneo la Mlima wakati ambao anaendelea kupigwa vita na viongozi vijana.

“Ni mwanzo wa awamu nyingine ya vita dhidi ya Gachagua ambaye amekuwa akihimiza umoja wa viongozi wa eneo la Mlima Kenya akinuia kujikweza kama msemaji wa kisiasa wa eneo hilo,” akaeleza Njenga na kuongeza kuwa kwa kiasi fulani, kujiunga kwa Waiguru na kinyang’anyiro cha urais kunaweza kubadilisha mwelekeo wa siasa za Mlima Kenya na nchi kwa jumula.

Bi Ngilu anasema wanawake wako na kila sifa inayohitajika kuongoza Kenya huku ikiibuka kuwa viongozi hao wanawake wanalenga wadhifa wa naibu rais katika uchaguzi mkuu wa 2027 kwa kuwa inaweza kuwa mlima kupata urais.

“Wanawake wa Kenya wana kile kinachohitajika kutoa rais. Waiguru, kwa kuwa umetimiza miaka kumi ya ugavana, ni kiti gani kingine kikubwa zaidi utakachowania. Usiulize ni kipi. Hakuna mtu mwingine mwenye uzoefu zaidi yako. Umekuwa gavana na waziri. Na kwa hivyo hupaswi kuogopa kusonga mbele kwa sababu una kile kinachohitajika,” Bi Ngilu alisema.

Mwakilishi wa Wanawake wa Kajiado, Bi Leah Sankaire ambaye ni afisa mkuu katika bodi ya ushauri ya G7, alifichua kuwa magavana hao wanawake wanalenga nafasi ya naibu rais katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

“Kama wanawake wa Kenya tunasema nchi iko tayari kwa naibu rais mwanamke,” akasema.