Jinsi Kalonzo atafaidika na masaibu ya Gachagua
ENDAPO juhudi za aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua za kutumia mahakama kurejea afisini zitagonga mwamba, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka anaonekana kama ndiye atafaidika kisiasa.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanabashiri kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba Bw Kalonzo ndiye atarithi ngome ya kisiasa ya Bw Gachagua 2027.
Hii ni kwa sababu kulingana na katiba ya sasa, kiongozi aliyeondolewa afisini kutokana na mashtaka hawezi kuruhusiwa kushikilia nyadhifa zozote za umma.
Mnamo Alhamisi, Oktoba 24, Mahakama Kuu inatarajiwa kutoa mwelekeo kuhusu kesi iliyowasilishwa na Gachagua kupinga kubanduliwa kwake.
Kulingana na Herman Manyora iwapo Bw Gachagua atagonga mwamba mahakamani, atasalia tu mwanasiasa asiyeweza kuwania au kuteuliwa kashikilia wadhifa wowote, hatima iliyopata magavana wa zamani Mike Sonko na Ferdinand Waititu.
“Kwa hivyo, endapo Gachagua hatafaulu mahakamani bila shaka hawezi kuwania kiti chochote katika uchaguzi mkuu ujao. Ndiposa Kalonzo anaonekana kama mgombea urais atayefaidi kisiasa haswa kwa kura za eneo la Mlima Kenya Magharibi,” Bw Manyora anaeleza.
“Hii ndio maana kiongozi huyo wa Wiper amekuwa mstari wa mbele kumtetea vikali Bw Gachagua tangu alipoanza kudhulumiwa, kisiasa, ndani ya Kenya Kwanza,” anaongeza.
Mnamo Ijumaa Bw Musyoka aliwakaripia vikali Spika Moses Wetang’ula na Spika wa Seneti Amason Kingi kwa kile alichotaja ni kuongozwa na nia mbaya “kuharakisha mchakato wa kutimuliwa kwa Bw Gachagua.”
“Mbona Seneti na Bunge la Kitaifa zilimsulubisha kisiasa haraka hata baada ya kujulishwa kwamba anaugua. Hii ni kinyume cha Katiba na haki za kibinadamu,” Bw Musyoka akawaambia wanahabari baada ya kumtembelea Bw Gachagua katika Hospitali ya Karen, ambako alilazwa akipokea matibabu.
Itakumbukwa kwamba kabla ya hoja ya kumtimua Bw Gachagua kuwasilishwa katika Bunge la Kitaifa, kiongozi huyo wa Wiper aliwaonya wabunge wa chama hicho dhidi ya kuiunga mkono.
Wabunge hao, 23, wakiongozwa na naibu kiongozi wa wachache Robert Mbui (Kathiani), walitii amri hiyo kwani walikuwa miongoni mwa wabunge 44 waliopiga kura ya LA kwa hoja hiyo.
Aidha, aliwaagiza maseneta wanne wa Wiper watupilie mbali mashtaka yote 11 dhidi ya Bw Gachagua, agizo ambalo walitii.
“Kalonzo alifanya hivyo ili kuimarisha uhusiano wa kisiasa kati yake na Gachagua. Hii ni licha ya kwamba alifahamu fika kwamba wabunge na maseneta wa wanaogemea mrengo wa Rais Ruto na Raila Odinga ni wengi na wangepitisha hoja hiyo kwa urahisi,” Bw Manyora anaongeza.
Kwa upande wake, Profesa Gitile Naituli anasema kuwa endapo Bw Gachagua hatapata “ukombozi” mahakamani Bw Musyoka yuko katika nafasi bora zaidi ya kurithi kura za eneo la Mlima Kenya Magharibi na hivyo kuboresha azma yake ya urais 2027.
“Hii inatokana na sababu kwamba kuna dalili kwamba Rais mstaafu Uhuru Kenyatta atamuunga mkono. Dalili hizo zilianza kuonekana mwezi Mei 2023 pale Bw Kenyatta alipozuru eneo bunge la Mwingi Kaskazini na kumhimiza Kalonzo awe mstari wa mbele kupalilia umoja ndani ya Azimio,” anaeleza.