Makala

Kalonzo angoja sauti ya Uhuru ili avune kura za Mlima 2027

Na CHARLES WASONGA November 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka sasa ndiye anapigiwa upatu kurithi eneo la Mlima Kenya Magharibi kisiasa kufuatia kutimuliwa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua japo  kibarua kinamsubiri kufikia hilo.

Sababu ni kwamba kwa mujibu wa kipengele cha 75 (3) cha Katiba ya sasa Bw Gachagua hawezi kushikilia wadhifa wowote wa umma kwa njia ya kuchaguliwa au kuteuliwa.

Sababu ni kwamba aliondolewa afisini kwa tuhuma za ukiukaji wa katiba miongoni mwa makosa mengine yanayohusiana na utovu wa maadili.

Naye Bw Musyoka, ambaye ni mmoja wa vinara wa Azimio, amekuwa mtetezi sugu wa Bw Gachagua tangu masaibu ya kisiasa yalipoanza kumzonga kiasi cha kuahidi kushirikiana na mbunge huyo wa zamani wa Mathira kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Kabla ya hoja ya kumtimua Gachagua kupigiwa kura katika Bunge la Kitaifa mnamo Oktoba 8, Kalonzo aliamuru wabunge wote 23 wa Wiper kuipinga.

Wabunge hao wakiongozwa na naibu kiongozi wa wachache bungeni Robert Mbui (Kathiani) ni miongoni mwa wabunge 44 waliosimama na Gachagua kwa kupiga hoja hiyo iliyopitishwa na jumla ya wabunge 282.

Hoja hiyo ilipotua katika Seneti, Kalonzo alishikilia uzi huo huo alipowaamuru maseneta wanne wa Wiper waipinge.

Ilivyo sasa ni kwamba wakazi wa eneo hilo wanahisi kusalitiwa na Rais William Ruto ambaye, kulingana na wao, ndiye alichochea hatua hiyo kwa sababu Gachagua alikuwa mstari wa mbele kutetea masilahi yao.

Hawajaridhishwa na hatua ya Rais Ruto kumtunuku Kithure Kindiki, anayetoka Mlima Kenya Mashariki, kiti cha Bw Gachagua wakishikilia kuwa wao ndio walichangia idadi kubwa ya kura milioni 3.5 alizopata kiongozi wa taifa kutoka eneo pana la Mlima Kenya katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Hadi wakati alipotimuliwa afisini, Bw Gachagua alikuwa amejijengea himaya kubwa ya ufuasi katika Mlima Kenya Magharibi linaloshirikisha kaunti za Nyeri, Murang’a, Kiambu, Kirinyaga, Laikipia na Nakuru.

Inakadiriwa kuwa eneo hilo lilichangia angalau kura milioni 2.5 kwenye kapu la Rais 2022, huku eneo la Mlima Kenya Mashariki likichangia angalau kura milioni 1.2. Mlima Kenya Mashariki linashirikisha kaunti za Embu, Meru na Tharaka Nithi, anakotoka Naibu Rais mpya Profesa Kithure Kindiki.

“Ni kweli Kalonzo sasa ndiye atarithi ngome ya Gachagua kisiasa kwani amekuwa mtetezi wake tangu mchakato wa kumwondoa afisini ulipoanzishwa. Kwa hivyo, kiongozi huyo wa Wiper anatarajia kufaidi kutokana na kura za wakazi wa Mlima Kenya Magharibi kuelekea 2027 atakapowania urais,” anasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Herman Manyora.

Lakini anamwonya Kalonzo katika kibarua cha kunasa kura hizo takriban milioni 2.5 hakitakuwa rahisi kwani kando na Gachagua, atahitaji uungwaji mkono kutoka kwa mtu kama Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

“Kalonzo atahitaji kumvutia Uhuru upande wake, sasa ambapo rais huyo mstaafu wamerejelea shughuli zake za kawaida. Kuna uwezekano mkubwa zaidi kwamba wakazi wa uliokuwa Mkoa wa Kati sasa watamtii ushauri wa Uhuru kuhusu ni nani wanafaa kumuunga mkono katika kinyang’anyiro cha urais,” Bw Manyora anaeleza.

Katika uchaguzi mkuu wa 2022, wakazi wa eneo hilo walimkaidi Bw Kenyatta alipowashauri kumpigia kura Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga.

Waliamua kumpigia kura Rais Ruto, wakati huo akiwa Naibu Rais, kwa wingi na kumwezesha kushinda.