MakalaSiasa

KINAYA: ‘Baba’ asisubiri hisani ya Uhuru aambiwe akalie kigoda cha ikulu!

May 6th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na DOUGLAS MUTUA

‘BABA’ ametongozwa akatongozeka, lakini atakula huu na hasara juu! Aliyemtongoza pia atakula huu. Lakini hii haitakuwa mara ya kwanza kwa ‘Baba’ kujaribisha ujanja wa kisiasa na kuambulia patupu.

Inashangaza hajajifunza chochote tangu anoe alipoingiza tingatinga tumboni mwa jogoo akitarajia Mzee Kirungu apaliwe na moshi wa tingatinga, akohoe kishenzi na kumwambia ‘chukua kigoda cha ikulu ukalie!’

Ni heri ‘Baba’. Anayemtongoza sasa hajui kwamba hajui. Wanasiasa hujiambia wanapendwa sana, hakuna mwingine kama wao, ila siku ya siku ikifika huaibishwa.

Ikiwa ‘Ithe wa Jaba’ anajidanganya kwamba angali maarufu katika uliokuwa mkoa wa Kati, basi anaota mchana hali yu macho. Huko kulitokwa mwaka jana.

Sasa hawezi hata kuwashawishi wenyeji wamchague mtu yeyote mwenyekiti wa josho la ng’ombe kwao kijijini Ichaweri.

Watu walinidhani kichaa miaka kadha iliyopita nilipoandika kwamba iwapo Baba Jimmy angeamua kumrithisha ‘Baba’ urais mnamo 2013 angekuwa peke yake.

Hata Mama Jimmy na nyumba yake yote hawangekubali kumpa kura ‘Baba’. Kisa na maana? Hawamtambui, kwao huyo ni mtu wa kelele nyingi asiyeaminika.

Hiyo ndiyo ‘injili’ ambayo watu wengi wa pale mlimani wamejua tangu enzi za mababu zetu, mengineyo hawatambui.

Hivyo basi kwa mtu kudhani anaweza kubadilisha hali hiyo ni kujidanganya, yaani kung’ata mnofu mkubwa hali hajajaaliwa meno makubwa na makali kuutafuna.

Wakati huo niliandika kuhusu ugumu wa Agwambo kuungwa mkono huko kwani wakati fulani tulipokuwa na serikali ya muungano Baba Jimmy alionekana kumpenda sana.

Baba Jimmy alipodhani mtu bora zaidi kumrithi alikuwa MaDVD, wadau wa siasa za mlimani walijitokeza na kusema”‘ng’o! ni ‘Kamwana’ pekee, Mzee upende usipende…”

Baba Jimmy hakufanya chochote kwa maana yeye mwenyewe alikuwa mlezi wa ufalme tu, wenye mamlaka katika ufalme huo ni wengine na ndio huamua.

Ni kwa mintaarafu hiyo ambapo ningali naangua kicheko, nusura mbavu ziniteguke, kwa wapayukaji kudai kura ya maamuzi ili tuunde wadhifa wa waziri mkuu.

Wakenya si wapumbavu; kila wakati ukitaja ‘waziri mkuu’ wanajua ni ‘Baba’ anayetafuta kuingia ikulu kupitia mlango wa nyuma.

Najua ni hoja ambayo inaweza kuungwa mkono zaidi na wafuasi wa ‘Baba’, hasa kina yakhe ambao hufuata upepo kama bendera.

Lakini inaweza kutumika na kina mwana wa mlimani kumwaibisha mwenzao anayestaafu; mkataba wake nao ulikamilika mwaka jana alipochaguliwa tena.

Kuanzia sasa, maamuzi ya hatima ya siasa za mlima Kenya si yake kabisa. Yeye sasa ni wa kuketi na kuambiwa, yaani kuwasikiliza wadau wakuu, asipopenda akajinyonge!

Watu wa mlimani wameapa hata kwa dawa hawawezi kukubali tuwe na wadhifa wa waziri mkuu, sikwambii wameungana na wenzao wa Bonde la Ufa katika msimamo huo.

Akitaka kustaafu vibaya, ‘Ithe wa Jaba’ ajaribu kuandaa kura ya maamuzi kuhusu wadhifa wa waziri mkuu. Atashindwa vibaya, aiache nchi katika kilele cha uhasama na taharuki.

Wabunge wakiungana kuwaundia watu nyadhifa zisizo kwenye Katiba, waikwepe kura ya maamuzi, watakataliwa kwa fujo mashinani ifikapo 2022. Hii Kenya si ya mama ya mtu!

 

[email protected]