Makala

Mfalme Uhuru Kenyatta kimya Mlima Kenya ukiporomoka kisiasa

Na BENSON MATHEKA October 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

HUKU Naibu Rais Rigathi Gachagua akionekana kuporomoka kisiasa na Mlima Kenya ukigawanyika, macho yote yanaelekezwa kwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kuona iwapo atatoa mwelekeo utakaodumisha umoja wa eneo hilo.

Baada ya Bw Gachagua kushindwa kushawishi eneo hilo kumkubali kama msemaji wa kisiasa, alimtambua Bw Kenyatta kama mfalme wa Mlima Kenya, akamuomba msamaha kwa kumshambulia wakati wa kampeni na kusema wakazi watafuata mwelekeo atakaowapa rais huyo mstaafu.

“Uhuru ndiye mfalme wa kisiasa wa Mlima Kenya na hatutatumiwa tena kumdharau na kumtusi mfalme wetu. Tutakuwa tukifuata mwelekeo wake wa kisiasa kuendelea mbele,” Bw Gachagua amekuwa akisema baada ya uhusiano wake na Rais William Ruto kuingia baridi.

Huku Bw Gachagua akikabiliwa na tishio la kuondolewa kama naibu rais miaka miwili baada ya Kenya Kwanza kuingia mamlakani, Bw Kenyatta amekuwa kimya hata wakati ngome ya kisiasa aliyounganisha kwa zaidi ya miaka kumi inaposambaratika.

Kabla ya hoja ya kumtimua Bw Gachagua ofisini kuwasilishwa katika Bunge la Kitaifa, nyufa zilijitokeza eneo la Mlima Kenya wabunge wa kaunti tatu za Meru, Embu na Tharaka Nithi wakijitenga na Bw Gachagua na kumuidhinisha waziri wa usalama wa ndani Prof Kithure Kindiki kama msemaji wao.

Japo wenzao kutoka Mlima Kenya Magharibi walifuata nyayo zao siku chache baadaye katika kile ambacho wadadisi wanasema yalikuwa maandalizi ya kumkaanga Gachagua, ilikuwa wazi kuwa ulikuwa mkakati wa kugawanya eneo hilo ili kulinyima nguvu na usemi wa kisiasa.

Wachanganuzi wa kisiasa wanatilia shaka kauli ya Bw Gachagua kwamba alizika tofauti zake na Bw Kenyatta wakisema kuwa rais huyo mstaafu au familia yake hajajitokeza hadharani kuthibitisha madai ya mbunge huyo wa zamani wa Mathira.

“Kimya cha uhuru licha ya Gachagua kusema mara kadhaa kwamba walizika tofauti zao hasa wakati huu ambao Mlima Kenya unagawanyika kisiasa ni ishara kwamba tofauti zao zingalipo. Masaibu ya sasa ya kisiasa ya Mlima Kenya yanatokana na uasi ambao wakazi walimuonyesha Uhuru wakiongozwa na Gachagua na washirika wa Rais Ruto kutoka eneo hilo,” asema mchanganuzi wa siasa Joe Mwiria.

Kutokana na uasi huo, wakazi walikataa kufuata ushauri wa Uhuru na kuunga Rais Ruto na Bw Gachagua katika uchaguzi mkuu uliopita huku wakiwachagua wabunge wengi wa chama chao cha United Democratic Alliance (UDA).

Dkt Mwiria anasema hata wakazi wakimlilia Bw Kenyatta kuwapa mwelekeo wa kisiasa, masaibu ya sasa ni suala la chama cha UDA ambayo si mwanachama. “ Itakuwa kama kuingilia ugomvi wa ndoa ya watu wengine ambao walikudharau wakisema ulikuwa ukipinga uchumba wao na hata wakajaribu kubomoa nyumba yako Gachagua na Ruto walivyofanyia chama cha Jubilee,” asema.

Baada ya kuingia mamlakani, serikali ilianza juhudi za kuharibu chama cha Jubilee huku ikifadhili baadhi ya wabunge kumbandua Uhuru uongozini mkakati ambao wachanganuzi wa siasa wanasema ulilenga kunyima eneo la Mlima Kenya chombo chenye nguvu cha kisiasa kinachoweza kupatia UDA upinzani.

Mirengo miwili iliibuka katika chama cha Jubilee, mmoja ukiongozwa na mbunge wa Afrika Mashariki Kanini Kega na mbunge mteule Sabina Chege kama katibu mkuu na kiongozi mtawalia na mwingine ukiongozwa na Uhuru, Katibu Mkuu Jeremiah Kioni na David Murathe kama naibu mwenyekiti.

Baada ya mvutano wa miaka miwili, wiki hii mahakama iliamua washirika wa Uhuru ndio maafisa halali wa Jubilee na kumrejeshea rais huyo mstaafu uthibiti wa chama hicho.

Inatarajiwa kuwa baada ya vumbi linalotifuka UDA kutulia na mzozo kuhusu uongozi wa chama cha Jubilee ukiisha, Bw Kenyatta atajitokeza kama mfalme wa Mlima Kenya na kupatia eneo hilo mwelekeo wa kisiasa.

Bw Kioni anasema “viongozi wa Jubilee tayari wamejipanga kisiasa ili kukipa umaarufu chama hicho” katika kile ambacho wachanganuzi wanaamini kuwa kinalenga kutumia hali ya sasa isiyoridhisha wengi Mlima Kenya ikiwemo masaibu ya Gachagua.

Alifichua kwamba Bw Kenyatta alifurahishwa na uamuzi huo, akisema kuwa “Uhuru anafurahi kwamba ukweli na haki zimeshinda. Hajawahi kuwapinga waasi na hana nia ya kufanya hivyo.”