Vyakula vya kipekee wanandoa wanaweza kuandaa kipindi hiking cha Krismasi
KWA wanandoa wengi, msimu wa Krismasi ni muda wa kupumzika, kuungana na familia na kuunda kumbukumbu ya kipekee jikoni.
Lakini mara nyingi, shinikizo la kupika vyakula vingi kwa wageni au familia husababisha mivutano isiyofaa.
Ndiyo maana mtaalamu wa lishe Christine Oduor anashauri wanandoa kupanga mlo mapema na kuchagua vyakula rahisi, vya bei nafuu.
Kwanza, Bi Christine anawashauri wanandoa kuandaa nyama choma yenye ladha ya kipekee, wakitumia viungo vinavyopatikana kwa urahisi kama tangawizi, kitunguu saumu, pilipili manga na limau.
Kuunda aina hii ya chakula ni rahisi na kinaweza kupikwa na wote wawili—mmoja akichoma huku mwingine akitengeneza kachumbari safi yenye nyanya, vitunguu, pilipili hoho na chumvi.
Mchanganyiko huu si tu rahisi bali pia wenye afya na unaongeza mandhari ya sherehe.
Pili, wali wa nazi au pilau ni chaguo bora kwa familia nyingi nchini kipindi cha sherehe.
Ili kuondoa msongamano jikoni, wanandoa wanaweza kugawana majukumu: mmoja apike wali huku mwenzake akitengeneza kitoweo kama kuku wa nazi, maharagwe ya kupaka ama mboga za kienyeji kama mchicha na sukuma wiki.
Mboga hizi husaidia kupunguza gharama na kuongeza virutubisho muhimu mwilini.
Kwa upande wa vitafunwa, mkate wa ndizi (banana bread) au maandazi ya vanilla yanaweza kutayarishwa mapema na kuhifadhiwa.
“Haya yanafaa watoto na wageni wanaofika bila kutarajiwa. Wanandoa wanaweza kufanya shughuli hii pamoja kama namna ya kuimarisha ukaribu, hasa kwa kucheka na kufurahia harufu tamu ya mkate unapoiva,” anasema Bi Christine.
Vinywaji pia ni muhimu katika msimu wa Krismasi. Badala ya kutumia hela nyingi kununua soda, wanandoa wanaweza kutengeneza juisi asilia za passion, embe, ndimu au matunda yaliyopo nyumbani.
Juisi hizi ni nafuu, bora kiafya na ni njia nzuri ya kutumia matunda yanayopatikana kwa wingi msimu huu.
Bi Christine pia anasisitiza umuhimu wa kuandaa chakula kwa kiasi ili kupunguza uharibifu.
Hivyo anawahimiza wanandoa kupanga idadi ya wageni na aina ya chakula mapema. Kwa kufanya hivyo, watakuwa na muda zaidi wa kufurahia sherehe na si kukimbizana jikoni.
“Kumbukeni kuwa siri ya Krismasi ni ushirikiano, ubunifu na furaha. Wanandoa wanaotumia muda huu kuandaa chakula pamoja huimarisha penzi lao na kuunda kumbukumbu zitakazodumu,” anaongeza.