Makala

Sababu za magavana kutisha kusitisha shughuli za kaunti

Na STEVE OTIENO November 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAGAVANA wamesema watasitisha shughuli za kaunti baada ya siku 30 iwapo mabunge yatakosa kuelewana kuhusu kiwango cha fedha kinachofaa kutumwa kwa magatuzi hayo.

Akizungumza baada ya kusimamia mkutano maalum wa Baraza la Magavana (COG) jijini Nairobi, Mwenyekiti Ahmed Abdullahi amesema, wamekasirishwa na Bunge la Kitaifa kusisitiza kuwa ni Sh380 bilioni zitatumwa kwa kaunti, na si Sh400 bilioni kama ilivyopendekezwa na Seneti.

Licha ya mabunge kupitisha Mswada wa Kaunti wa Ugavi wa Mapato, miezi mitano baadaye bado Sheria hii haijaidhinishwa na hivyo kusababisha kaunti kukosa kupokea mgao wa mapato katika mwaka huu wa kifedha 2024/25.

Gavana Abdullahi alidokeza kuwa licha ya kaunti kuathiriwa na uhaba wa fedha, serikali ya kitaifa inaendelea kupokea mgao wake baada ya Bunge la Kitaifa kupitisha Sheria ya Matumizi ya Ziada ya 2024.

“Baraza la Magavana linapinga uamuzi wa Bunge la Kitaifa kupunguza mgao sawa wa mapato kwa Sh20 bilioni,” akasema Bw Abdullahi.

“Tunathibitisha na kuunga mkono uamuzi wa Seneti kukosa kubadilisha mgao wa kaunti uwe Sh400 bilioni… kupunguzwa kwa mgao kwa Kaunti utaathiri vibaya utoaji huduma na kusimamisha shughuli za kaunti,” aliongeza.

Magavana walikosoa Bunge la Kitaifa kwa kuzingatia bajeti ya ziada kwa kigezo cha Mswada wa Marekebisho ya Ugavi wa Mapato (DORA) wakisema kuwa bajeti hiyo haitokani na Sheria ya Ugavi wa Mapato ya 2024.

Vile vile, magavana walishikilia, hali kuwa Sheria ya Ugavi wa Mapato inatokana na hesabu zilizo katika Mswada ambao uko mbele ya kamati ya upatanishi katika Bunge, inafanya Sheria ya Matumizi ya Ziada ya 2024 kuwa kinyume cha Katiba.

Walinukuu ushauri uliotolewa na Mahakamu ya Juu 2019 ambao ulisema Bunge haliwezi kupitisha Mswada wa Matumizi ya Ziada kabla ya kukamilishwa kwa Mswada wa Ugavi wa Mapato.

Wakuu wa kaunti wamekashifu Bunge la Kitaifa wakisema wanalemaza ustawi wa ugatuzi kama inavyotakiwa na katiba.

Kwa kutokuwepo kwa Sheria ya Ugavi wa Mapato kwa Kaunti, magatuzi yamekuwa yakipokea hadi asilimia 50 ya mapato sawa kutokana na bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2023/2025.

Kufikia Desemba, mgao huu utaisha na kuacha kaunti zikiwa na matatizo ya kifedha Januari 2025.

Taarifa iliyosambazwa na Hazina ya Kitaifa imeonyesha kuwa katika miezi ya Juni, Julai, Agosti na Septemba, kaunti zilipokea Sh30.8 bilioni, 32.7 bilioni, 30.8 bilioni na 32.7 bilioni mtawalia, ambazo ni jumla ya Sh158.02 bilioni zilizotolewa kwa kaunti katika mwaka huu wa kifedha.