SHINA LA UHAI: Corona si hatari tu kwa afya bali pia mazingira
Na LEONARD ONYANGO
VIDEO ya mwanaume aliyeonekana akisafisha barakoa/maski zilizotumika iliwatia hofu Wakenya ilipochipuza katika mitandao ya kijamii miezi miwili iliyopita.
Katika video hiyo, mwanaume huyo alionekana akifua rundo la barakoa zilizotumika kwenye maji machafu yanayoaminika kuchotwa ndani ya Mto Nairobi.
Kwa mujibu wa ripoti, mwanaume huyo aliokota barakoa zilizotumika karibu na hospitali ya Mbagathi, jijini Nairobi ambapo wagonjwa wa virusi vya corona wanatibiwa, na kwenda kuzisafisha kabla ya kuziuza tena.
“Niliona mtu akisafisha barakoa alizookota katika eneo la Gikomba na kisha kuziuza tena,” akasema mtumiaji wa mitandao ya kijamii, Lilian Wambui.
Wakenya sasa wanahofia kuwa huenda baadhi ya barakoa zinazouzwa mitaani zikawafanya kuambukizwa virusi vya corona badala ya kuwakinga.
Uchunguzi uliofanywa na Jarida la Afya Jamii katika mitaa mbalimbali ya Nairobi ulibaini kuwa takataka ya barakoa zilizotumika imetapakaa kila mahali.
Wataalamu wa afya na wanaharakati wanasema kuwa uchafu huo wa barakoa na glovu zilizotumika huenda ukasababisha virusi vya corona kusambaa zaidi.
Shirika la la Umoja wa Kimataifa kuhusu Mazingira (UNEP) limeonya kuwa janga la corona litasababisha kuongezeka kwa maelfu ya tani za takataka ambayo ni hatari kwa afya na mazingira.
Shirika hilo linasema kuwa takataka hizo zinajumuisha barakoa, glovu na vifaa vya matibabu vilivyotumiwa katika kuzuia maambukizi ya virusi hivi.
Ripoti kuhusu Hali ya Uchumi nchini ya 2020 iliyotolewa na Shirika la Takwimu (KNBS) miezi miwili iliyopita inaonyesha kuwa serikali za kaunti tayari zimelemewa na kiasi kikubwa cha takataka zinazozalishwa katika miji mbalimbali nchini.
Jijini Nairobi, kwa mfano, kiasi cha takataka kiliongezeka mwaka 2019 kutoka tani milioni 2.7 mnamo 2018 hadi tani milioni 2.9.
Serikali ya Kaunti ya Nairobi ilifanikiwa kuzoa asilimia 55.3 ya takataka hizo na kuacha asilimia 45.7 ya uchafu umetapakaa mitaani.
Kati ya tani 320,000 za takataka zilizozalishwa jijini Mombasa mwaka jana, ni tani 147,000 tu zilizokusanywa na serikali ya kaunti.
Serikali ya Kaunti ya Kisumu ilifanikiwa kuzoa tani 63,000 tu kati ya tani 210,000 za uchafu uliozalishwa jijini humo.
Wataalamu wanasema kuwa janga hili litasababisha serikali za kaunti kulemewa zaidi hivyo kuwatia wakazi katika hatari ya kupatwa na Covid-19 kutoka kwa barakoa, glovu na vifaa vinginevyo vilivyotumika.
Kuna hofu kuwa uchafu wa barakoa na glovu zilizotumika huenda ukasababisha ongezeko la maambukizi huku mitaa ya mabanda ikitarajiwa kuathirika zaidi.
Ripoti ya sensa ya 2019, inaonyesha kuwa mitaa ya mabanda inaongoza kwa kutupa takataka kiholela bila kuzingatia kanuni za usafi.
Asilimia 42.6 ya wakazi wa mtaa wa Kibra, ambao unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya maambukizi ya corona jijini Nairobi, hutupa takataka barabarani, mitaroni au vyanzo vya maji.
Asilimia 20.1 na asilimia 15.1 ya wakazi wa mtaa wa Mathare na Starehe mtawalia, hutupa takataka zao za nyumbani kiholela katika vyanzo vya maji, mitaro ya kupitisha maji taka na barabarani.
Mathare ni miongoni mwa mitaa iliyo na idadi kubwa ya waathiriwa wa corona jijini Nairobi.
Aidha ripoti hiyo inaonyesha kuwa asilimia 7.8 ya familia milioni 1.5 zilizoko jijini Nairobi, hutupa takataka za nyumbani ovyoovyo barabarani na mitaroni. Familia hizo ndizo huchangia kwa kiasi kikubwa katika uchafuzi wa Mto Nairobi.
Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa takribani familia 20,000 jijini Mombasa zinatupa takataka za nyumbani kiholela.
Nchini Kenya, kuna jumla ya kaya milioni 12 lakini ni asilimia 6.3 tu ambazo takataka zao huzolewa na serikali za kaunti.
Katibu mkuu wa shirika la kutetea mazingira la United Green Movement, Hamisa Zaja, anasema kuwa utupaji ovyo wa barakoa na mavazi mengineyo ya kukinga virusi vya corona kunaweza kusababisha maradhi hayo kusambaa zaidi, haswa katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu.
Bi Zaja anasema idadi kubwa ya Wakenya hawana ufahamu kuhusu njia salama za kutupa barakoa, glovu au mavazi mengineyo ya kuwakinga dhidi ya kuambukizwa corona.
“Wakati huu wa janga la virusi vya corona, idadi kubwa ya Wakenya wanatumia barakoa na glovu kujikinga dhidi ya maambukizi. Lakini baada ya kuzitumia hawajui mahali pa kupeleka takataka hizo,” anasema.
Bi Zaja anaitaka serikali kuimarisha juhudi za kuwaelimisha Wakenya kuhusu njia mwafaka za kutupa uchafu unaotokana na vifaa au mavazi ya kuzuia maambukizi.
James Wambugu ambaye ni muuzaji wa barakoa jijini Nairobi, anasema kwamba amekuwa akijaribu kuwaelimisha wateja wake kuhusu njia mwafaka za kutupa zilizotumika lakini wengi wao wanapuuzilia mbali ushauri wake.
“Serikali inafaa kuhamasisha umma kuhusu jinsi ya kukusanya uchafu wa barakoa ili usije ukasambaza zaidi corona,” anasema.
Tafiti ambazo zimefanywa zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya Wakenya wanaamini kuwa kuvalia barakoa ni njia mojawapo ya kuzuia maambukizi.
Utafiti uliofanywa na KNBS mwezi uliopita ulionyesha kuwa asilimia 79 ya Wakenya wanaamini kuwa wakivalia barakoa wanazuia kusambaa kwa virusi hivi.
Utafiti uliofanywa na shirika la TIFA jijini Mombasa na Nairobi pia ulionyesha kuwa asilimia 3 ya Wakenya wanaamini kuwa kuvalia glovu kunawakinga dhidi ya corona.
Mwongozo wa Nema kuhusu utupaji taka
Katibu wa Wizara ya Mazingira na Misitu Chris Kiptoo anasema kuwa wananchi wanafaa kufuata mwongozo wa Mamlaka ya Uhifadhi wa Mazingira (Nema) kuhusu njia mwafaka za kutupa barakoa au vifaa vya kujikinga na virusi vya corona.
Dkt Kiptoo anasema kuwa utupaji kiholela barakoa au vifaa vinginevyo vya kimatibabu ni hatari kwa mazingira na afya ya binadamu.
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, mnamo Aprili alikiri kuwa kuna changamoto ya utupaji takataka ya vifaa ya kujikinga na virusi vya corona kama vile barakoa na glavu.
Bw Kagwe, hata hivyo, alisema kuwa serikali imeandaa mwongozo kuhusu njia salama za kutupa takataka hizo bila kuhatarisha mazingira na afya ya watu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Nema Mamo Boru Mamo, anasema kuwa barakoa na glovu ni miongoni mwa vitu vilivyowekwa kwenye kundi la takataka hatari zinazoweza kusababisha maradhi.
“Asilimia 85 ya takataka zinazotokana na vifaa vya kimatibabu huwa hazina madhara. Lakini asilimia 15 ni hatari kwa afya kwani zinaweza kuwa na virusi, bakteria, sumu na hata zinaweza kulipuka,” anasema Bw Mamo.
“Baadhi ya vifaa vya kujikinga na virusi vya corona kama vile barakoa na glovu hutumika mara moja na kisha kutupwa. Hali hiyo imesababisha ongezeko la takataka nchini. Iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa, basi huenda kukawa na maambukizi zaidi ya virusi vya corona na uchafuzi wa mazingira,”anaongezea.
Anasema kuwa barakoa, glovu na vifaa vinginevyo vya kujikinga na corona vinajumuishwa katika kundi la takataka za hospitalini hivyo vinafaa kutupwa kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya 1999.
Kulingana na mwongozo wa Nema; barakoa, glovu, chupa za sabuni na dawa ya kuua viini (sanitaiza) hazifai kuchanganywa na takataka nyingine nyumbani.
“Virusi vya corona vinaishi kwa siku nyingi juu ya vitu kama vile barakoa au glovu hivyo unapotupa takataka ndani ya nyumba au njiani, sokoni, nje ya dirisha la matatu, na kadhalika, unahatarisha maisha ya wengine,” anasema Bw Mamo.
Hata hivyo, anakiri kuwa idadi kubwa ya Wakenya hawana mazoea ya kutenganisha takataka na wamekuwa wakitupa kiholela.
“Kuchanganya barakoa na takataka nyinginezo za nyumbani kunatia hatarini watu ambao huokota chupa na vitu vingine katika majaa,” anasema.
Mwongozo wa Nema unahitaji wamiliki wa nyumba za kupanga kuweka jaa, linalofunguliwa kwa miguu kuwezesha wapangaji kutupa hapo takataka hatari kama kama vile barakoa zilizotumia.
Matatu na afisi pia zinafaa kuwa na majaa hayo spesheli ya kutupa takataka zinazoweza kusababisha maambukizi ya maradhi.
Katika maeneo ya vijijini, Nema inahitaji serikali za kaunti kusambaza majaa ya kukusanya takataka zinazoweza kusababisha maambukizi katika afisi za machifu, sokoni au eneo lolote linaloweza kufikiwa na watu wengi.
Bw Mamo anasema kuwa nyumbani, haswa katika maeneo ya vijijini, takataka zilizo na barakoa zinafaa kunyunyuziwa kemikali ya Sodium hypochlorite na kisha kutumbukizwa kwenye shimo la choo.
Ripoti ya Sensa 2019 inaonyesha kuwa asilimia 3.6 ya familia, ambazo ni sawa na familia 434,000, kote nchini hutupa takataka ndani ya shimo la choo.
Marufuku ya serikali
Serikali mnamo Aprili ilipiga marufuku watu kuabiri magari ya umma, kwenda madukani, sokoni au kuabiri bodaboda bila kuvalia barakoa.
Mtu anayepatikana na hatia ya kuvunja sheria hiyo anatozwa faini ya Sh20,000 au kifungo cha miezi sita gerezani.
Barakoa zimejizolea umaarufu kutokana na ukweli kwamba zimesaidia kupunguza maambukizi ya virusi vya corona kote duniani.
Shirika la WHO linasema kuwa watu wanapozungumza, kukohoa, kuchemua au kucheka wanatoa mate ambayo yanaweza kuwa na virusi vya corona ambavyo husalia hewani kwa muda mrefu.
Shirika la WHO linapendekeza kuwa watu wasio na barakoa watumie katarasi shashi au kitambaa wanachoweza kutupa mara baada ya kukohoa au kuchemua.
Watu ambao hawajavalia barakoa wanapoenda katika eneo lililo na virusi vya corona hewani, wanaambukizwa hata baada ya waathiriwa kuondoka.
Hiyo ndiyo maana serikali sasa inataka kila mtu anayeenda nje ya nyumba yake kuvalia ili kujikinga.
Tafiti zilizofanywa zinaonyesha kuwa ni vigumu kuambukizwa corona iwapo utatangamana na mwathiriwa ikiwa nyote mmevalia barakoa.